March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wawili wa afya Nkasi wafukuzwa kazi kwa utoro

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi

‎Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilayani Nkasi mkoani Rukwa, limewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wawili wa kada ya afya kwa kuwafukuza kazi kwa sababu ya utoro wa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi.

‎Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao cha mashauri ya kinidhamu kilichoketiwa na Madiwani hao, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Richard Masai,amesema wamejiridhisha na taarifa za watumishi hao za kuwa watoro wa muda mrefu katika maeneo yao ya kazi, hivyo wanakila sababu ya kuwafukuza kazi ili iwe fundisho kwa wengine.

‎Watumishi waliofukuzwa kazi ni Lyangawe Charles Lutu muuguzi daraja la II kituo cha afya Kirando na Gaudensia Fredrick Lukago muuguzi msaidizi daraja II kituo cha afya Kabwe.

‎Pia Baraza hilo la Madiwani,limepitisha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa makadirio ya kukusanya na kutumia jumla ya shilingi billion 47.3.

‎Akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti,Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo,Steward Vidoga,amesema mapendekezo ya bajeti yamelenga kutekeleza shughuli mbalimbali za kutoa huduma za jamii, kuboresha miundombinu na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 100 ya makisio ya mwaka 2026/2027.

‎Aidha kupitia baraza hilo Madiwani wamejadili mapitio ya mpango na bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026, kuanzia Julai hadi Desemba, ambapo wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji Afraha Hassan,kwa kusimamia mapato na shughuli mbalimbali za maendeleo kwakipindi ambacho hakukuwa na Baraza la madiwani.