NA Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DODOMA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu amewakumbusha watumishi wa ofisi yake kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuyafikia malengo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao chake na watumishi wa ofisi hiyo kilichofanyika Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 23, 2023.
Katibu Mkuu huyo amesema upo umuhimu wa kujizoeza kupima afya hususan kwa magonjwa sugu yasiyoambuiza kwani yameendelea kuwa changamoto hasa kwa watu wenye umri mkubwa.
“Ni muhimu tumepata fursa ya kukumbushwa kupima afya zetu, hii ni changamoto inayotukabili, hivyo ni muhimu kuzingatia ushauri wa afya na masharti ya namna ya kuboresha masuala yanayohusu afya zetu, “amesema Dkt. Yonazi
Pamoja na hilo amewakumbusha watumishi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuendelea kutekeleza majukumu wakiwa wenye afya na kuwa na matokeo chanya.
Aidha ametumia mkutano huo kuwaasa watumishi hao kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Mkutano huu ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo tulianza kuiadhimisha tarehe 16 Juni, 2023 na leo ndio kilele.Wiki hii tunaitumia kutafakari namna tunavyotekeleza majukumu yetu kwa kipindi kilichopita, kujadili namna ya kutoa huduma bora kwa jamii ya Watanzania, kujifunza mbinu mpya na kuibua changamoto zinazotukabili katika kutekeleza majukumu yetu kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi,”amesisitiza
Pia amewahimiza Watumishi kuendela kufanya kazi kwa upendo na kuheshimiana kwani kwa kufanya hivyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani.
“Ni falsafa yangu kuona watu ninaowaongoza wanafanya kazi kwa upendo na kushirikiana, ni lazima kuhusiana na kuwa na mashirikiano mazuri, napenda kufanya kazi na watu wanaoheshimiana na wenye amani siamini kama mtu anaweza akafiri vizuri iwapo hana amani ndani”amesisitiza Dkt. Yonazi
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti ya TUGHE wa Ofisi ya Waziri Mkuu Numpe Mwambenja alipongeza uwepo wa mkutano huo huku akieleza kuwa ni nyenzo muhimu kwa kuongeza motisha kwa watumishi wa umma, na imeonesha kujali na kuendelea kuleta umoja kazini.
“Mkutano huu umekuja wakati sahihi na muda sahihi, tunawapongeza viongozi wetu kuendelea kutuweka pamoja na kutukumbusha kupendana, kushirikiana na kuishi kwa amani, hili tumelithamini sana na tunaahidi hatuta waangusha tutachapa kazi na kuendele kuhudumia jamii ya Watanzania na kuitumikia nchi yetu kwa ujumla,”amesema Numpe.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu