June 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa afya Pangani watakiwa kutanguliza utu

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

MKUU wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala amewataka Watumishi wa Afya wilayani humo kutanguliza utu badala ya maslahi ya fedha mbele ambayo yanaweza kusababisha madhara kwa wagonjwa huku akiwaasa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa weledi.

Mkuu huyo ameyasema hayo Juni 24,2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Kilakala amefafanua kwamba wapo wananchi wengine wanakwenda kutibiwa wakiwa wameshikika na ugonjwa, hivyo kumuuliza fedha badala ya kumtibu yanaweza kutokea madhara yanayosababisha baadae watu kuanza kunyoosheana vidole.

“Mtu amekuja na mnamuona anahitaji kutibiwa kwa haraka kwanza kabla ya fedha msisubirie msaidieni, madaktari na wauguzi mara kadhaa nimewaelekeza, watibieni hawa wananchi ili wasipoteze maisha, mimi Mkuu wenu nipo tutasaidiana,” ameeleza na kuongeza kuwa

“Tusipoteze wananchi wetu,kwasababu ya fedha, yale mambo yaliyotokea katika Wilaya zingine na mikoa mingine katika huduma za afya, tunajipanga ili katika Wilaya yetu ya Pangani yasiendelee kutokea,”.

Amesisitiza watumishi hao kutoa kipaumbele kwa wajawazito, wakina mama wenye watoto wachanga pamoja na wazee, ambapo kadi zao zinapaswa kutumika, ili wapatiwe matibabu.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya huyo amesema wamejipanga kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kwani ukusanyaji wake ni mdogo hivyo wamechukua jitihada za makusudi katika kipindi cha kuelekea miezi sita kuhakikisha wanakusanya zaidi.

“Tumeamua kumuunga mkono Rais wetu kutoka kwenye nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi, hili ni azmio kutoka mwaka 2024 hadi 2034, kwa Mkoa wa Tanga, Wilaya hii imeona fursa ya kwenda kuwekeza katika hewa ya ukaa,”

“Ili Halmashauri yetu ipate mapato mengi, tutahakikisha tunapunguza wimbi la ukataji wa miti ovyo katika maeneo yetu, tukishakuwa na biashara ya hewa ya ukaa vijiji vitajitegemea na kuwa na miradi mikubwa ya maendeleo,” amesema.