March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi Mbarali wahimizwa kufanya kazi kwa weledi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbarali

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imewataka watumishi wake kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uzalendo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Wito huo umetolewa Desemba 19, 2025 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, mara baada ya kikao kazi kilichowakutanisha wakuu wa idara na vitengo pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mweli amesema kikao hicho kililenga kuhimiza misingi ya utawala bora, ushirikiano, uzalendo na kuheshimu utawala wa sheria katika utekelezaji wa majukumu ya kila mtumishi.

“Tulikuwa na kikao muhimu kati ya Mheshimiwa Mbunge na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri yetu. Ajenda kuu ilikuwa kuhimiza watumishi kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji, uzalendo na kuzingatia utawala wa sheria,” amesema Mweli.

Mweli ameongeza kuwa kikao hicho pia kilisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani kama kipaumbele cha halmashauri, akieleza kuwa katika mwaka wa fedha uliopita halmashauri ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 10, mapato yaliyotokana zaidi na mazao.

Amebainisha kuwa bado zipo fursa nyingi za vyanzo vya mapato ambavyo havikuwa vikikusanywa ipasavyo licha ya kutambuliwa kisheria, vikiwemo vibali vya ujenzi, leseni za biashara, ushuru wa mabango na kodi za taka.

“Vyanzo hivi vipo kisheria lakini havikuwa vikifanya vizuri. Tumesisitiza kila chanzo kinachotambulika kisheria kikusanywe ipasavyo kwa kushirikiana na wakuu wa idara, watendaji wa kata na vijiji,” amesema.

Amesema zoezi la usimamizi na uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato tayari limeanza katika maeneo ambayo awali hayakuwa yakifanya vizuri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi bila upendeleo.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi na watumishi ni nguzo muhimu ya maendeleo na kwamba dhamira ya pamoja na uwajibikaji vitawezesha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo yanayotarajiwa na wananchi wa jimbo hilo.

Mkazi wa kata ya Lugelele, Tabia Bakari, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali imeanza kuonesha mabadiliko chanya kiutendaji, akieleza kuwa mkurugenzi wa sasa amekuwa akiwashirikisha watumishi katika masuala mbalimbali ya maendeleo.