November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi Hospitali ya Rufaa Mbeya wapewa mafunzo ya mfumo mpya wa manunuzi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Mbeya imeanza kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu mfumo mpya wa manunuzi wa Nest, ambao unalenga kuboresha na kufanya manunuzi ya hospitali hiyo kwa rahisi, haraka na uwazi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Idara ya Ugavi – MZRH ,Denis Mtasiwa amesema kuwa uongozi wa hospitali umeratibu mafunzo kutolewa kwa watumishi wa ngazi mbalimbali.

Ambapo watumishi hao ni pamoja na idara ya manunuzi,fedha na mipango kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanajua jinsi ya kutumia mfumo huo mpya kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa mfumo wa manunuzi wa Nest unatumia teknolojia ya kisasa ya mtandao na unaruhusu watumishi wa hospitali hiyo kufanya manunuzi kwa njia ya mitandao,inamaanisha kuwa manunuzi yanaweza kufanyika kwa haraka na kwa uwazi zaidi.

Mtasiwa ameeleza kuwa Serikali imewekeza kwenye mfumo huo mpya wa manunuzi ambao utasaidia kupunguza matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha kuwa manunuzi yanafanyika kwa njia ya uwazi,kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi.