November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa wa wizi washambuliwa na wananchi

Judith Ferdinand, TimesMajira Online MwanzaWatuhumuwa wawili wa wizi katika matukio tofauti wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wameshambuliwa na wananchi wenye hasira kali kwa mawe na silaha za jadi na baadae kupoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa tukio la kwanza mnamo Machi 24,2023,majira ya saa 5:30(23:30)katika soko la Buhongwa Kata ya Buhongwa mtu aitwaye Hakimu Joseph, mwenye umri wa miaka 24, Msukuma, Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, alikamatwa na kushambuliwa na wananchi baada ya kumkuta amekata bati la nyumba na kutoboa cellingboard.

Kisha kuingia kwenye duka la kuuza pembejeo za kilimo la Aziza Sadick, mfanyabiashara, Nyakagwe Buhongwa na kuiba kiasi cha Tsh. 600,000( laki sita) pamoja na simu ndogo aina ya Nokia ya kutolea huduma ya M-Pesa.

SACP.Mutafungwa, ameeleza kuwa mbinu iliyotumiwa na mtuhumiwa kutekeleza uhalifu wake, ni kwamba Machi 22,2023 mchana mtuhumiwa alifika katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DELIGHT ambayo jengo lake limeunganishwa na maduka 5 (fremu) ambayo yako mkabara na barabara ya Mwanza/Shinyanga.

Ambapo ilipofika usiku alitoboa cellingboard na bati kisha kuingia kwenye duka (fremu) la kuuzia pembejeo za kilimo na kuiba kiasi hicho cha fedha kisha alianza kutoboa ukuta wa duka (fremu) la kuuza simu za mkononi na vifaa vyake mali ya Baraka Segeno, mkazi wa Buhongwa.

Akiwa anaendelea kutoboa ukuta, ndipo Baraka Segeno ambaye alikuwa amejifungia ndani kwake akifanya mahesabu alisikia kishindo na kutoa taarifa kwa wamiliki wengine wa maduka akiwemo Aziza Sadick, na walipofika duka la kuuza pembejeo za kilimo lilifunguliwa ndipo mtuhumiwa alipitia kwenye tundu la cellingboard aliyokata awali.

Kisha na kuanza kukimbia kwenye paa la nyumba hiyo kwa lengo la kukwepa kukamatwa, hata hivyo, wananchi wenye hasira kali walimshambulia kwa mawe na kudondoka chini.

“Askari wetu waliokuwa kwenye doria eneo hilo waliwatawanya wananchi hao kisha kumkamata mtuhumiwa huyo na kumpeleka katika Hospitali ya Bugando kwa matibabu kwasababu hali yakeilikuwa mbaya kutokana na kipigo, pamoja na jitihada za kuokoa maisha yake mtuhumiwa alipoteza maisha akiwa anaendelea kupatiwa matibabu,”.

Vile vile ameeleza kuwa mtuhumiwaalikutwa na vifaa vya kuvunjia, simu yake ya mkononi aina ya Momofly na madawa ya kienyeji.

Katika tukio jingine lililotokea Machi 24,2023 majira ya saa 9:30(15:30) mchana katika mtaa wa Ihila, Kata ya Buhongwa, wananchi walimkamata mtuhumiwa mmoja aliyefahamika kwa jina la Devid Deogratius,mwenye umri wa miaka 32,Mkazi wa Mtaa wa Nyanembe,Kata ya Buhongwa.

Na kumshambulia kwa silaha za jadi baada ya kumkuta akiwa amevunja nyumba ya Octavius Eustace @ Mulokozi, Mwalimu, Shule yaMsingi Kirumba na Mkazi wa Ihila ‘A’ kwa kupitia dirishani na kuiba Tv Flat screen aina ya Sumsung.

Katika tukio hilo, Askari waliokuwa doria walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa tayari amejeruhiwa na wananchi kisha kumkimbiza katika Hospitali ya Bugando.

Ameeleza kuwa pamoja na jitihada hizo zilizofanyika ili kuokoa maisha yake, mtuhumiwa alifariki akiwa anapatiwa matibabu.

“Katika tukio hilo mtuhumiwa alikutwa na vifaa vya kuvunjia na baada ya kupitiakumbukumbu zake za kiuhalifu tumebaini kwamba alitoka Gereza la ButimbaMachi 22,2023 kwa dhamana na kosa lake ni wizi Criminal case no 182/2023,”ameeleza SACP.Mutafungwa.