March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa 46 wa makosa mbalimbali wakamatwa Dar

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar-es-Salaam,limewakamata watuhumiwa 46 kwa tuhuma mbalimbali za makosa ya jinai yakiwemo ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, kuvunja godown, stoo na kuiba.

Pia limewakamata watuhumiwa wengine wanaofanya biashara za kununua mali za wizi zikiwemo simu, runinga, pikipiki, kompyuta mpakato(laptop) na redio.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Februari 24,2026,Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar-es-Salaam,SACP Jumanne Murilo aliwataja watuhumiwa hao
ni pamoja na Rashidi
Mtunguja “msambaa” na wenzake wanne wakazi wa eneo la Jangwani wilayani Ilala.

Pia amesema wamemkamata, Issa
Nassoro ‘Kurukutu’ na wenzake wawili wakiwa eneo la Gongolamboto wilayani Ilala.Pia walimkamata Nicolaus Abdallah mkazi wa Manzese akiwa na wenzake wanne.

Aidha ameongeza katika msako huo walimkamata, Khalid Stephano ‘Kiswili’ wa Temeke na wenzake wawili kwa
tuhuma za wizi wa tableti na vifaa vya mtandao vyenye thamani ya shilingi
milioni 400 mali ya Kampuni ya SCI Tanzania Ltd.

Amesema baada kufanya matukio hayo walidaiwa kutumia gari namba T457CQF aina ya Noah nayo inashikiliwa na jeshi hilo kwa kuhusishwa na matukio
ya kijinai yakiwemo ya kubeba mali za wizi.

Katika hatua nyingine Kamanda Murilo amesema pia wamekamata pikipiki 20 zinazodaiwa kuibwa maeneo tofauti jijini humo,simu 110 na vifaa mbalimbali vinavyotumika kufanyia uhalifu huo.

Amesema Polisi Kanda Maalumu ya Dar-es-Salaam kupitia Ofisi za Mashitaka na Mahakama za kisheria
jijini imepata mafanikio ya kisheria baada ya watuhumiwa mbalimbali kati ya waliokamatwa kuanzia Januari 30 hadi Februari 24,2026 kupatikana na hatia baada ya
ushahidi kutolewa mahakamani.

“Waliopata adhabu ni pamoja
na Mwita Marwa na wenzake wawili wakazi wa Kigamboni walihukumiwa
kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kosa la
kubaka kwa kundi,”amesema

Mwingine ni Morisi John Ngaleje mkazi wa Kibada alihukumiwa na
Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka.

Pia Adam Sanilo mkazi wa Kibada alihukumiwa na Mahakama ya
Wilaya ya Kigamboni kifungo cha miaka 60 jela kwa kosa la unyang’anyi wa
kutumia silaha na kubaka.

Naye Athumani Said mkazi wa Buza alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la
unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kamanda Muliro ameongeza kuwa naye Nurdin Jafari mkazi wa Chang’ombe
alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kifungo cha miaka 30 jela
kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, Mohamed Omary mkazi wa
Mbande alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya Temeke kifungo cha maisha
jela kwa kosa la kubaka.