Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online, Shinyanga
WATOTO wawili na watu wengine wawili wa familia moja wakazi wa kijiji cha Mwalata, Kata ya Shagihilu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa na fisi aliyevamia katika makazi yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambalo limetokea usiku wa kuamkia Jumatatu ya Januari 30, 2023 fisi huyo amewajeruhi watoto hao sehemu mbalimbali za miili yao.
Mashuhuda hao wamewataja watoto ambao wamejeruhiwa na fisi huyo kuwa ni Kanizio Joseph ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Lazaro Emmanuel pia mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Mwalata na ndugu zao wengine wawili Jishanga Izengo (18) na Malambi Mayala.
Imeelezwa kuwa fisi huyo aliwavamia wanafamilia hao usiku wakati wakiwa wanalinda mifugo yao mbuzi na ng’ombe waliokuwa nje kwenye zizi.
Mama mzazi wa watoto waliojeruhiwa ambaye amejitambulisha kwa jina la Mbuke Jishanga amesema watoto wake walivamiwa na fisi mnamo saa saba usiku wakiwa kwenye lindo la kulinda mifugo hiyo.Mbuke amesema,
“Mnamo saa saba za usiku nilimsikia kijana wangu Jishanga akipiga kelele hivyo nilitoka nje nikakuta wanashambuliwa na fisi, nilishituka sana ikabidi nikimbilie panga na kuanza kuwasaidia wanangu kwa kumpiga fisi huyo huku tukipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani,”
“Bahati nzuri majirani walifika huku nikiwa nimefanikiwa kumkata kwa panga fisi huyo sehemu za kichwani na akawa ameanguka chini ambapo majirani pia waliendelea kumpiga mpaka akafa,” ameeleza Mbuke.
Mbuke amefafanua kuwa kutokana na shambulio la fisi huyoJishanga amejeruhiwa sehemu ya chini ya pua yake, Kanizio yeye kajeruhiwa sehemu za mapajani, Lazaro ameumizwa maeneo ya kichwani na mikononi pamoja na Malambi ambaye kajeruhiwa sehemu za kichwani na shingoni na wote walikimbizwa hospitali ambako wametibiwa na kushonwa majeraha yao.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kishapu Dkt. Mohamedi Mkumbwa amethibitisha kuwapokea majeruhi wote mnamo saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu ya Januari 30, 2023 wakiwa na hali mbaya na walipatiwa matibabu kwa kushonwa maeneo waliyojeruhiwa na hivi sasa wanaendelea vizuri.
More Stories
Baraza la wazee Kata ya Kilimani laahidi kampeni nyumba kwa nyumba
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba