November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu milioni 296 duniani wanaishi na maambukizi sugu ya virusi vya homa ya Ini aina B

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

IMEELEZWA kuwa watu wapatao milioni 296 duniani wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina B na watu milioni 58 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina C.

Barani Afrika kuna Watu milioni 60 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina B na Watu milioni 10 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina C.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Julai 24,2024 na Mkuu wa Programu za UKIMWI,Ngono,Ini,Malaria,Kifua Kikuu,Uelimishaji mifumo ya afya,Dkt.Catherine Joakim wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maadhimisha ya Siku ya Homa ya Ini Duniani.

Yenye lengo kuongeza uelewa wa homa ya ini ambao husababisha ini kuvimba na hivyo kupelekea uwezo mkubwa wa kupata ugonjwa kwenye ini au kansa ya ini.

Amesema kuwa kwa Tanzania inakadiriwa kiwango cha ushamiri wa ugonjwa wa Homa ya Ini ni asilimia 3.5 (aina B) na asilimia 1 (aina C) Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani za mwaka 2021.

Dkt.Joakim amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ugonjwa wa homa ya ini ikiwemo,kujumuisha huduma za homa ya ini pamoja na magonjwa ya ngono kwenye uliokuwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa UKIMWI (NACP).

“Na hivi sasa mpango huo unajulikana kama NASHCoP,Mpango huu ulizinduliwa mwezi Novemba mwaka 2023,”amesema.

Aidha Kuimarisha upatikanaji wa chanjo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya
,Kuimarisha upatikanaji wa matibabu ya homa ya ini, Kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa homa ya ini

Napenda kutoa rai kwa wananchi kutumia fursa ya huduma hizi kwa kupata huduma za kujikinga pamoja, uchunguzi na tiba.

Dkt.Joakim ameeleza kuwa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Homa ya Ini yamepangwa kufanyika Sinza darajani, Uwanja wa TP, Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 hadi 28 Julai, 2024 kuanzia saa 02:00 asubuhi yatakayokwenda sambamba na utoaji wa Elimu kuhusiana na Virusi vya Homa ya Ini, VVU na lishe, Upimaji wa maambukizi ya Chanjo za homa ya Ini, Kuunganishwa na matibabu baada ya kukutwa na maambukizi, Upimaji wa VVU,Upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza(kisukari na shinikizo la damu).

Yanayokwenda na Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2024 inayosema “Ni Wakati wa Kuchukua Hatua ikiyataka mataifa kuongeza kasi na juhudi makusudi katika huduma za kinga, uchunguzi na tiba ili kupunguza vifo vitokanavyo na maambuki ya virusi vinavyosababisha homa ya ini”.

Kilele cha maadhimisho haya kitakuwa tarehe 28 Julai,2024 ambapo huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Mwisho