December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 9 wafariki kwa ajali mlima Iwambi Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WATU tisa wamepoteza maisha mkoani Mbeya baada ya dereva wa lori lenye namba za usajili BCE 9384/ABX8675 kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali wa Mbalizi na kwenda kuigonga gari ya abiria yenye
namba za usajili T.636 DQY aina ya Mitsubish Rosa .

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea Septemba 22 mwaka huu majira ya saa 11.40 jioni katika eneo la mteremko wa Iwambi wilayani Mbeya Vijijini mkoa wa Mbeya .

Kamanda Kuzaga amesema kuwa gari yenye namba za usajili BCE 9384/ABX 8675 aina ya Howo mali ya kampuni ya Horn Afric Motors ltd ya nchini Zambia ikitokea Mbeya kuelekea Tunduma likiendeshwa na dereva Mohamed Abilah (47) Mkazi wa Zambia .

Aidha Kuzaga ameeleza kuwa gari hilo iliigonga kwa nyuma Gari yenye namba za usajili T.636 DQY aina ya Mitsubish Rosa ikitokea Mbeya mjini kuelekea Mbalizi ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva ,Elly Mwakalindile (41)mkazi wa Iyunga na kusababisha vifo vya watu tisa kati yao wanaume watano na wanawake wanne.

Amesema kuwa katika ajali hiyo watu 23 walijeruhiwa kati yao wanaume 13 na wanawake 10 wanaoendelea kutibiwa katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi na wengine wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi Mbalizi ambapo miili 7 imetambuliwa huku miwili ikiwa bado haijatambuliwa.

Chanzo cha ajali hii ni Dereva wa lori kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali na kwenda kuigonga kwa nyuma gari ya abiria na kuwa Dereva wa lori amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa madereva ambao wanapita katika Mkoa wa Mbeya kwenye milima na miteremko mikali kuhakikisha wanakagua magari yao kabla ya kuanza safari na wamiliki wa magari wasiruhusu magari yao kuendeshwa na madereva hao ili kuepusha ajali.