Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WATU 50 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na vurugu zilizosababisha watu wawili na polisi watatu kujeruhiwa zilizotolewa wilayani Magu mkoani Mwanza
Vurugu hizo zinadaiwa kutokea baada ya gari moja la abiria kuwagonga wanafunzi wawili waliokuwa wakitembea kwa miguu wakivuka barabara ya Mwanza-Musoma na kusababisha kifo na kumjeruhi mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 12,2023 kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema wanawashikilia watu 50 kwa tuhuma za kuhusika kufanya vurugu, kupanga mawe barabarani, kuharibu mali na kuwajeruhi abiria waliokuwa wakisafiri kwa gari hilo.
Amesema ajali hiyo imetokea Agosti 11, mwaka huu, majira ya saa 1:30 asubuhi,katika mtaa wa Nyalikungu A, Kata ya Magu Mjini barabara ya kutokea Mwanza kwenda Musoma,iliohusisha gari lenye namba za usajili T 121 DCU Toyota Hiace, mali ya Boniface Joseph, mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza iliyokuwa inatoka Magu kuelekea Mwanza.
Mutafungwa amesema gari hilo lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Musoma lilipofika eneo la Nyalikungu liliwagonga wanafunzi wawili waliokuwa wakitembea kwa miguu wakivuka barabara katika kivuko cha waenda kwa miguu.
Aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Consolata Marwa (10), mwanafunzi wa darasa la tano na mkazi wa Manyasini na Magreth Ntemi (12) mwanafunzi wa darasa la tatu na mkazi wa Magu, wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyalikungu wilayani Magu.
“Gari hilo liliwagonga wanafunzi wakati wakivuka katika alama ya pundamilia na kuwasababishia majeraha sehemu mbalimbali za miili yao,majeruhi hao walikimbizwa kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu bahati mbaya Consolata Marwa alifariki dunia ambapo Magreth anaendelea na matibabu,”amesema Mutafungwa.
Amesema mara baada ya ajali hiyo kutokea Askari Polisi wa Wilaya ya Magu,walifika eneo la tukio kushughulikia ajali hiyo,wakati wakiwaondoa majeruhi pamoja na gari lililosababisha ajali kuruhusu mengine yapite,wananchi walishinikiza gari hilo lichomwe moto.
Mutafungwa ameeleza kuwa askari hawakukubaliana na shinikizo hilo ambapo wananchi hao waliwarushia askari mawe na magari yote yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo, waliweka vizuizi barabarani na kuchoma moto matairi.
Ameleza kuwa kufuatia vurugu hizo abiria wawili na askari polisi watatu walijeruhiwa huku magari sita yakiharibiwa ambapo askari wengine kutoka polisi Magu walifika eneo hilo kuongeza nguvu katika eneo la ajali ili kubidhiti vurugu na uharibif
“Baada ya kutokea kwa vurugu hizo askari polisi wengine walifika eneo la tukio kwa haraka kwa ajili ya kuongeza nguvu na kulazimika kutuliza ghasia hizo kwa kuwatawanya wahalifu hao na kuhakikisha hali ya usalama ya eneo hilo inaimarika na tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 50 waliokuwa wakifanya fujo na uharibifu huo wa mali za wananchi ambapo hali ya amani ilirejea muda mfupi,”.
Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kutojali watumiaji wengine wa barabara na kutoheshimu alama za barabarani ambapo polisi inaendelea na juhudi za kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ambaye amekimbia kusikojulikana baada ya kusababisha ajali hiyo.
Aidha aliwataka wananchi kuheshimu kanuni,taratibu na sheria za nchi na kutojihusisha kwa namna yoyote na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kuwaadhibu wanaofanya makosa mbalimbali kuwa jeshi hilo halitasita kuwachukua hatua za kisheria.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato