November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 31 wapandikizwa figo BHM kiasi cha fedha bilioni 2.3 zaokolewa matibabu nje ya nchi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma.

HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BHM) imefanikiwa kupandikiza figo kwa watu 31 na kuokoa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi billion 2.3 huku ikitibu watu 715 ugonjwa wa Moyo na kati yao 39 walibainika na matatizo ya moyo nakuwekewa vipandikizi na kati yao 8 wamepandikiziwa betri kwenye moyo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Benjamini Mkapa Dkt.Alphonce Chandika wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa vipaumbele vya hospitali hiyo kwa Mwaka 2022/2023.

Ambapo amesema gharama ya huduma hiyo kwa Hospitali  hiyo ni takribani sh. milioni 25 wakati nje ya nchi mgonjwa angetibiwa kwa takriban Sh. milioni 100.

Aidha amesema Hospitali imefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo ambapo kuna maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua.

“Hospitali hii ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hii.Tangu huduma hii imeanza kutolewa mwaka 2019, jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa,” .

Na kuongeza”Wagonjwa  39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha,” amesema Dkt,Chandika.

“Kuna  wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo,”amesema Dkt Chandika

Aidha amesema Hospitali imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo ambapo tayari watoto kumi wameshahudumiwa.

Hata hivyo ameeleza tangu mwaka 2020, Hospitali ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya shilingi milioni 12. Gharama za huduma hii nchi za nje ni takriban milioni 35.

Amesema Kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa jumla ya Shilingi bilioni 1.28

“Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia  mgonjwa upasuaji, huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7,”amesema

Dkt Chandika amesema Kwa wagonjwa 148,  Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850.

Pamoja na hayo Dkt.Chandika ametaja huduma zilizoanzishwa ndani ya Serikali ya awamu ya sita ambapo ameeleza
wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19, hospitali ilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba ‘oxygen’ , Serikali ilitupatia Shilingi bilioni 1.1 na  milioni 400 zilitokana na mapato ya ndani kwa ajili ya  kununua na kusimika mtambo wa kuzalishia hewa tiba, kununua mitungi 560 na gari la kusambazia hewa tiba hiyo katika Hospitali mbalimbali, jumla mradi umegharimu shilingi bilioni 1.5

“Mtambo huo una uwezo wa kuzalisha mitungi 400 ndani ya masaa 24, tangu mtambo huu uzinduliwe, Julai 1, 2022, jumla ya mitungi 13,467 imeshazalishwa ambapo mitungi 10,962 imetumiwa hospitali hapa na mitungi 2,505 ilisambazwa kwenye Hospitali zenye mahitaji,” .

“Uzalishaji  wa mitungi hii Hospitalini hapo ndani ya kipindi kifupi, umeokoa zaidi ya Shilingi milioni 500 na imeongeza mapato ya ndani ya hospitali kwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 75 ambazo Hospitali zingine zinachangia kwa kupelekewa huduma hii,” amesema Chandika.