November 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 2,000 kuungana kuliombea Taifa, Rais Samia Mbeya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

ZAIDI ya wananchi 2,000 wanatarajiwa kushiriki kongamano maalumu la kuliombea Taifa amani na utulivu, litakalofanyika Novemba 20, 2026, jijini Mbeya, likiwahusisha viongozi wa dini mbalimbali na wananchi.

Akizungumza Novemba 13, 2026, katika mkutano wa kuhamasisha kongamano hilo uliohusisha wenyeviti wa mitaa 181 ya Jiji la Mbeya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kupitia Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, amesema maandalizi yanaendelea na wananchi wameanza kuhamasishwa kujitokeza kwa wingi.

Mwaselela amesema kongamano hilo litawakutanisha viongozi wa dini mbalimbali pamoja na waimbaji, kwa lengo la kuunganisha wananchi katika maombi ya pamoja ya kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.

“Hii ndiyo kamati namba moja inayotoka katika mitaa yote ya Jiji la Mbeya, siku hiyo, Novemba 20, 2026, tutakwenda vizuri, wanakamati hawa wako tayari kuliombea amani Taifa letu na Jiji la Mbeya…. twendeni tukaombee amani,” amesema.

Amesema kongamano hilo litaanzia Mkoa wa Mbeya na baadaye kuhusisha wilaya zake, akieleza kuwa kupitia maombi hayo wanatarajia kuliweka Taifa, viongozi na wananchi mbele ya Mungu.

Ameongeza kuwa maombi hayo yatajumuisha kuliombea Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na maendeleo ya Mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga, Mary Komba, amesema kongamano hilo limeandaliwa kwa kutambua umuhimu wa amani na utulivu katika kufanikisha shughuli za maendeleo.

Amesema wameona ni muhimu kumshirikisha Mungu katika juhudi za kuimarisha amani, huku akiwataka vijana kuepuka kutumiwa vibaya na badala yake kushiriki katika shughuli zinazojenga umoja na mshikamano wa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Community Centre, Kata ya Maendeleo, Rachel Mwakipesile, amesema wenyeviti wa mitaa watatumia nafasi zao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo.

Amesema lengo ni kuwaunganisha wananchi katika maombi ya pamoja ili kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, utulivu na mazingira mazuri yatakayowezesha shughuli za maendeleo kufanyika.