January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 200 watibiwa macho Songwe

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Songwe

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Hellen Keller wamefanikiwa kuwatibu watu zaidi ya 200 katika huduma za mkoba za upasuaji wa mtoto wa jicho ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya za Macho kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 7, 2023 katika huduma za mkoba za upasuaji wa mtoto wa jicho na Meneja wa mradi huo Athuman Tawakali zilizofanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mkoani humo.

Tawakali amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za Afya katika upande wa macho ili kutoa huduma bora na kuzuia upofu kwa wananchi.

Aidha, Tawakali ameongeza kuwa shirika hilo litaendelea kuboresha huduma za mkoba za upasuaji wa mtoto wa jicho katika Mikoa mbalimbali kwani wahitaji wa huduma za Afya ya macho bado ni wengi nchini.

Hata hivyo Tawakali ameeleza huduma hizo zitaendelea katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Mbeya na Njombe ili kuboresha huduma ya afya ya macho kwa wananchi ambao hawawezi kumudu gharama za upasuaji wa mtoto wa jicho.

Tawakali ameendelea kwa kuishukuru Serikali ya awamu wa sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za wadau katika kuboresha huduma za Afya kupitia Wizara ya Afya.

Vile vile , ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa ambazo serikali kwa kushirikiana na wadau wanazitoa ili kuendelea kuboresha huduma bora za Afya nchini na kuhakikisha taifa linakuwa na afya bora.