Na Queen Lema, Times majira Arusha
Watoto zaidi ya 100 kutoka jijini Arusha wamefanikiwa kupatiwa elimu ya fedha pamoja na uwekaji wa akiba kutoka kwenye Chama cha Ushirika cha Arusha Women in Business saccos ltd(AWIB).
Hayo yameelezwa jijini Arusha na Meneja wa Chama hicho,Maria Maembe wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wiki ya taasisi za fedha.
Maria amesema kuwa watoto hao wamepata elimu hiyo ndani ya miezi sita iliopita ambapo mpaka sasa wameweza kuwa mabalozi wazuri wa namna ya kuweka na kuhifadhi fedha.
Amefafanua kuwa watoto hao ni wanachama wa chama hicho cha ushirika na mbali na kuweza kupewa elimu wameweza pia kujinunulia vitu na vifaa vyao ambavyo vinawasaidia katika michezo lakini hata kwenye masomo.
“Hawa watoto kila mara huwa tunakutana nao na tunawapa elimu juu ya matumizi sahihi ya kuhifadhi fedha na kuachana na tabia ya kutapanya fedha ovyo naniseme tu wameweza kuwa vinara wazuri mpaka sasa wamefikia malengo yao kwa kiwango cha juu,”amesema.
Ameeleza umuhimu wa kuwafundisha watoto kujiwekea akiba kuwa wanapopata elimu inawasaidia kutunza kile ambacho wanapewa na wazazi au ndugu kwa ajili ya matumizi ya baadae na kwa kuwajengea uwezo hivyo inawasaidia hata kuwa na akiba endapo tu kutakuwa na changamoto au ulazima wa kutumia akiba hiyo.
Mbali na hayo pia aliwataka wazazi hususani wanawake kuhakikisha kuwa wanajiunga na chama hicho ambacho mpaka sasa kimekuwa mkombozi kwa kuweza kutoa elimu lakini pia mikopo nafuu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya chama hicho Dkt.Nsia Urasa amesema kuwa watoto wanapofundishwa kutunza na kujiwekea akiba wakiwa wadogo inawasaidia kuepukana na matumizi yasiyo sahihi.
Amesema kuwa moja ya mkakati walio nao wao kama wadau wa ushirika ni pamoja na kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na maarifa sahihi lakini pia iweze kujiwekea akiba kwa ajili ya baadae.
Pia amesema kuwa chama hicho kimeweza kupata tuzo nyingi hasa kwenye maonesho ya kitaifa mbalimbali kwa kuwa wanatoa elimu lakini pia kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu