March 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto yatima 100 wapatiwa bima za afya Rorya

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara

MJUMBE wa Baraza kuu la Umoja wa Wanawake     (UWT) Taifa Mkoa wa Mara,Rhobi Samwelly amekabidhi Bima za Afya 100 za (CHF) kwa  watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu wanaolelewa na Kikundi cha ‘Pamoja  Tuwalee’kilichopo Shirati Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara ili kuhakikisha   watoto hao wanakuwa na uhakika wa matibabu wanapougua.

Rhobi amekabidhi Bima hizo katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo katika Wilaya ya Rorya  yamefanyika  Machi 6,2025 katika Viwanja vya Obwere Shirati na kuhudhuriwa na wananchi,wanafunzi wa shule mbalimbali za Msingi na Sekondari,Viongozi wa Mashirika pamoja na Serikali.

Akikabidhi Bima hizo kwa niaba ya Rhobi Diwani wa Viti maalumu kutoka Tarafa ya Inchage Wilaya ya Tarime,Nuru Hondi  amesema kuwa Rhobi ametoa Bima hizo  kufuatia ombi lililowasilishwa kwake na kiongozi wa Kikundi kinachowahudumia watoto hao Sylvana Ngemera kutokana na changamoto ya matibabu yaliyokuwa yanawakabili. 

“Nilipokea ombi la Bima za Afya nami nikaona ni vyema kuwasaidia watoto hawa yatima na wenye uhitaji.Nitoa wito pia kwa Jamii tuendelee kuwasaidia wahitaji katika maeneo yetu na pia kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia,”Hondi

Kwa upande wake Kiongozi wa Kikundi cha ‘Pamoja Tuwalee’ ambaye pia ni Diwani wa Tarafa ya  Nyancha   Wilaya ya Rorya Ngemera amemshukuru Rhobi kwa msaada huo kwani utasaidia watoto hao kupata matibabu kwa uhakika tofauti na awali. 

“Namshukuru Mbaraza Rhobi kwa kutusaidia Bima hizi za Afya ambazo zitakuwa mkombozi kwa kuwahakikishia huduma za matibabu watoto hawa ambao baadhi yao ni walemavu,wamekuwa wakipata tabu kupata huduma lakini kwa Sasa watahudumiwa vizuri.” amesema Ngemera.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Shelta Mang’era amesema kuwa, Halmashauri hiyo inashukuru Juhudi za kusaidia maendeleo zinazofanywa na Rhobi kwani zinamanufaa makubwa huku pia akihimiza wadau mbalimbali kusaidia makundi maalumu katika Jamii ambayo haina uwezo.

Aidha,amewaomba wanawake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu jukumu la malezi kwa watoto wao,pia kupinga kikamilifu vitendo vyote vya Ukatili wa Kijinsia ambavyo bado vinafanywa katika Jamii Sambamba na Kuwafichua wahusika mbele ya vyombo vya kisheria ili wachukuliwe hatua kali.  

Mkuu wa Wilaya ya Rorya Dkt.Halfan Haule amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanaungana pamoja na Serikali kukemea vitendo vya ulawiti na ubakaji ndani ya Wilaya hiyo kwani bado Vipo.  Huku akisisitiza pia watoto wa kike wasomeshwe na kwa ajili ya faida ya Jamii na Taifa kwa ujumla. 

Dkt.Haule pia amesema kuwa mchango wa wanawake katika maendeleo na uongozi ni mkubwa sana,hivyo amesema kila mmoja analojukumu la kuwapa ushirikiano mkubwa wanapotekeleza majukumu yao na Serikali Wilayani humo itaendelea kuwawezesha wanawake na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya nyanja mbalimbali.