Judith Ferdinand
Watoto wanaozaliwa na changamoto ya ugonjwa wa kichwa kikubwa(kichwa kujaa maji kupita kawaida) na mgongo wazi nchini hapa bado ni tatizo huku moja ya sababu ikiwa ni ukosefu wa madini ya folic acid.
Licha ya tatizo hilo lakini bado watoto hao wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kunyanyapaliwa na jamii,kufichwa ndani na hata baba zao kuwatelekeza na kuwaacha wakipata malezi ya upande mmoja wa mama tu.
Hii yote ni kwa sababu bado jamii ina imani potofu juu ya ugonjwa huo wakiamini ni laana na mambo mengi.
Takwimu zinaonesha kuwa katika nchi tano barani Afrika zenye watoto wengi wanaozaliwa na changamoto hiyo Tanzania ni ya tatu(3) ikitanguliwa na Algelia na Ethiopia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Juni mwaka 2022,mara baada ya kushiriki mbio zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa(MOI)kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa watoto 200,wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi zilizofanyika jijini Dar-es-Salaam.
Anaeleza kuwa nchini hapa kwa kila watoto 1,000, watoto watatu(3) wanazaliwa wakiwa na tatizo la mgongo wazi na kichwa kikubwa huku takwimu za watoto ambao huzaliwa kila mwaka hufikia takribani milioni 2, hivyo watoto takribani 6,000, kila mwaka uzaliwa wakiwa na tatizo hilo.
WAZAZI WANENA
Nilifunga safari hadi Nyumba ya Matumaini(Hope House),iliyopo Nyegezi jijini Mwanza, kilipo kituo hicho cha kusaidia watoto wenye tatizo la mgongo wazi na kichwa kikubwa wakati wakisubilia matibabu au kuhudhuria kliniki katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Nilipokelewa na wenyeji wangu ambaye ni Meneja Nyumba katika kituo hicho pamoja na baadhi ya wamama wenye watoto wenye matatizo hayo ambao wapo katika nyumba hiyo.
Wakati tukiendelea na mazungumzo ya hapa na pale nilivutiwa na mtoto mmoja ambaye alikuwa mchangamfu licha ya kuwa na changamoto ya kichwa kikubwa nikatamani kufahamu historia yake baada ya kubaini kuwa mtoto huyo wamezaliwa mapacha lakini yeye pekee ambaye ndio Doto anasumbuliwa na changamoto hiyo huku mwenzie Kulwa hakiwa ni mzima wa afya bila ya changamototo yoyote.
Mama wa mapacha hao wenye umri wa miaka miwili na miezi minnne anazungumzia ugonjwa wa kichwa kikubwa kwa pacha mmoja(Doto).
Rebeca Maliatabu mwenye umri wa miaka 38 ni mama wa watoto wanne akiwa na nzao tatu kwa maana ya nzao mbili mtoto mmoja mmoja huku nzao ya tatu akibahatika kuzaa watoto mapacha ambao ni wa kiume.
Anaeleza kuwa alijifungua mapacha hao vizuri ila baada ya miezi takribani 6, pacha mmoja ambaye ndiye Doto alianza kuchemka na kumpeleka kituo cha afya baada ya vipimo waliruhusiwa kurudi nyumbani lakini kichwa cha mtoto huyo kilianza kuongezeka ukbwa kuliko kawaida ndipo mme wake aliamua kumtelekeza na kuondoka na watoto wengine huku akimuachia mapacha hao.
Maliatabu naeleza kuwa kutokana na mme kumkibia aliamua kutafuta vibarua ili watoto wake wapate chakula kwani hata ndugu zake hawamsaidii kitu chochote ambapo baba na mama yake wamefariki hivyo hakuna mtu wa kumsaidia.
Ambapo anaeleza kuwa hali hiyo ni ukatili kwa watoto wake kwa sababu wanakosa haki zao za msingi ikiwemo malezi ya wazazi wote wawili na huduma mbalimbali kama chakula,malazi na huduma za afya kwa sababu wao hawana kosa wala hawakuomba kuzaliwa nao.
“Nyumba ninayoishi nilipewa na msamaria mwema baada na mme wangu kunikimbia kisa pacha mmoja kupata changamoto ya kichwa kikubwa ambaye tulimgundua baada ya kuumwa na kumpeleka hospitali ya Mugisi ambapo mbali na kuchemka alikutwa amepungukiwa maji mwilini ambapo fedha ya kunisaidia matibabu nilipewa Sista wa Kanisa Katoliki la Mugusi,”anaeleza Maliatabu.
Kutokana na hali hiyo alipata msaada kutoka hospitali hiyo baada ya mtoto wake kuandikiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambao nao walimuunganisha na kituo cha Nyumba ya Matumaini wakati akisubilia mtoto wake afanyiwe upasuaji.
“Mwanangu alifanyiwa upasuaji Januari 18,2023 na hali yake inaendelea vizuri baada ya kuruhusiwa lakini wakati tuliporuhusiwa na kufika nyumbani baada ya wiki mbili watoto wangu wote waliugua malaria lakini walipona kwa msaada wa wasamaria wema na hata nyumba ninayoishi nimesaidiwa na msamaria mwema tu,”anaeleza Maliatabu..
Hata hivyo anaeleza kuwa kuzaa mtoto mwenye changamoto kumesababisha baba yao kuwatelekeza na kukosa haki ya malezi na matunzo hali hiyo kimsingi ni ukatili kwa sababu wanakosa haki zao za msingi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imeainisha haki ya mtoto kuwa ni pamoja na kulelewa na wazazi, kupata mahitaji ya msingi kama chakula,chanjo,malazi,matibabu na vitu vingine.
“Tazama sasa watoto wanaishi katika maisha ya kukosa huduma kwa kutegemea msaada wa watu pamoja na kufanya vibarua ambavyo kimsingi havinipi kipato sahihi cha kuweza kumudu mahitaji yao,’’ anaeleza kwa uchungu mama huyo na kuongeza kuwa
Pia anaeleza kuwa kwa sasa watoto wake wote wanaendeleaje vizuri lakini changamoto ni lishe isitoshe hivyo nalazimika kwenda kwa watu wenye mashamba ya nyanya ambao umpa nyanya zao zenye ujazo wa ndoo ndogo ya lita 10 ambazo uzunguka nanzo mtaani kuuza kisha kupeleka fedha kwa wahusika nayeye kuchukua kiasi cha shilingi 1,000 ambayo anaenda kununua unga na sukari kwa ajili ya kuwakorogea uji.
“Wakati mwingine nashindwa kuwapatia fedha zao kutokana na kuuza kidogo kwani ninapo enda kuuza nakuwa nimewabeba watoto wangu mapacha mmoja mgongoni mwingine kifuani hali inayosababisha nachoka haraka hivyo najikuta natembeza umbali kidogo na kurejea nyumbani ambapo unakuta nimeuza nyanya kidogo,”.
OMBI KWA SERIKALI NA JAMII
Maliatabu anaiomba serikali na jamii kwa ujumla kumsaidia aweze kupata mtaji wa kufanya biashara pamoja na kupata nyumba ya kuishi yeye pamoja na watoto wake mapacha.
“Novemba mwaka huu nategemea kurejea Mwanza kwa ajili ya kliniki hospitali ya Bugando ili wajue maendeleo ya mwanangu ata nauli ya kutoka Shinyanga mpaka huko siju nitatoa wapi naomba serikali na jamii inisaidie,”.
Naye Sauda Juma mama wa mtoto mwenye tatizo la kichwa kujaa maji kupita kawaida,anaeleza kuwa baada ya kumleta mtoto hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu baba wa mtoto alimkataa mtoto huyo hivyo amelazimika kukaa kwenye kituo cha Nyumba ya Matumaini mkoani Mwanza badala la nyumbani kwake mkoani Kigoma kwani mme huyo alimtaka atafute baba mzazi wa mtoto huyo kwani yeye siyo wake.
Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya Mtoto inaeleza kuwa ni kinyume na sheria kufanya vitendo vya ubaguzi,unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto huku ikieleza kuwa mtoto ana haki kuishi,haki ya kuishi na wazazi wake,kupata huduma bora za matibabu kwa ajili ya ustawi wake,haki za huduma pekee za walemavu.
“Mme wangu hamtaki mtoto wetu anadai kwamba mtoto ameisha poteza gharama nyingi kwaio kama imeshindikana nimrudishe nyumbani,ananiambia kwamba kwani mtoto mmoja akifa kuna tatizo gani,na mimi namwambia siwezi kumuacha mtoto wangu haangaike wakati nguvu za kupambana zipo,” anaeleza Sauda na kuongeza kuwa
“Sielewi sababu za yeye kusema kuwa mtoto huyu siyo wake na wakati mwingine anawapigia simu nyumbani kwetu na kuwaeleza kuwa hawezi kunitumia fedha ingawa anazo kwa sababu mtoto siyo wa kwake,”.
Anaeleza kuwa kwa sasa mtoto huyo anasumbuliwa na kidonda sehemu ya haja kubwa ambapo baba uwezo anao ila kumuhudumia ndio hivyo hataki maana ata kupiga tu simu kuulizia hali ya mtoto hafanyi hivyo na anahangaika pekee yake kama mama bila msaada zaidi ni ule anaoupata kutoka katika kituo hicho.
Pia amewatia moyo wazazi wenye watoto ambao wana changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi hususani wanawake ambao wanatekelezewa watoto na wanaume zao kisa changamoto hiyo kuwa wapambane ili watoto wao wapate matibabu na kuweza kukua kama wengine kwani changamoto hiyo siyo laana.
Sanjari na hayo anaeleza sababu ya wazazi wa kiume kukimbia watoto waliozaliwa na changamoto hiyo ni zile imani potofu walizonazo kwani wamekuwa wakisema kuwa watoto wanaozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa uwa hawadumu wana kufa.
“Kwamba watapoteza gharama kubwa na ndicho kitu kikubwa ambacho kinasababisha wanaume wanawatelekeza watoto wenye chanagamoto hiyo kuwa tatizo hilo haliwezi kutibika na hata wakipona watoto wa hivyo hawawezi kuwasaidia kitu chochote hivyo wanahesabu kama hasara,”.
Hata hivyo anaomba elimu itolewe kwa jamii huku wazazi wakiondoa imani potofu juu ya watoto wanaozaliwa na changamoto hiyo ya kuwa hawawezi kukua kitu ambacho hakina ukweli wowote.
“sisi tunaoenda Bugando tunawaona watoto wanakua na wengine ni madaktari na semina kila siku tunapewa hivyo wanaume wache imani potofu kuwa watoto hao hawawezi kukua,”.
Aidha anaeleza kuwa baada ya changamoto ya mme wake kumkataa mtoto kituo cha Nyumba ya Matumaini kilimchukua na kumpa ajira ya kusaidia shughuli mbalimbali kituoni hapo ingawa ombi lake kwa wadau na serikali kumuwezesha mtaji ili aweze kufanya biashara.
Anaeleza kuwa kufuatia gharama za bima kwa watoto kupanda kutoka 50400 ya awali mpaka gharama ya sasa ameiomba serikali kuangalia upya jambo hilo kwani linawapa wakati mgumu ukilinganisha na kipato walichonancho na ikizingatiwa watoto wengi wenye changamoto hiyo wazazi wao wa kiume wamewakimbia huku asilimia kubwa wakitoka katika familia duni.
Naye mmoja wa wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tausi Shija kutokea Mpanda mkoani Katavi ameeleza kuwa,moja ya sababu ya kupata mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi ni kutokana na kuchelewa kuhudhuria kliniki kwani alianza mimba ikiwa na miezi mitano hivyo nilichelewa kunywa dawa za folic acid.
Huku akiomba serikali kuziwezesha hospitali za mikoa kuweza kutoa huduma ya matibabu ya watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi ili waweze kufikiwa wengi zaidi.
MENEJA NYUMBA YA MATUMAINI ANENA
Meneja wa Nyumba ya Matumaini Getruda Butondo,anaeleza kuwa kituo hicho kinapokea watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi pamoja na wazazi wao wakati wakisubilia huduma ya matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Huku changamoto iliopo ni kuwa wanapokea wazazi wengi ambao hawana uwezo wa kuwahudumia watoto wao wenye changamoto hiyo huku wengi wao ni wanawake ambao wanaume wao wamewakimbia na wamewatelekeza baada ya kuzaa watoto wenye changamoto hiyo.
Kama shirika linachukua jukumu la kuwasaidia wanawake hao ili kupata matibabu ya mtoto pamoja na huduma za malazi na chakula ambapo kituo hicho kimeanzishwa ili kusaidia wamama hao ambao wengi walikuwa wanakosa sehemu ya kulala wakati wakisubilia matibabu ya watoto wao katika hospitali ya Bugando.
Anaeleza kuwa tatizo hilo linasababishwa na ukosefu wa madini ya Folic Acid kwani wanawake wengi wanatoka katika familia duni hivyo unakuta hawapati chakula kwa muda na chenye virutubisho vyote wakati wanapokuwa wajawazito.
Huku wengine wanachelewa kwenda kliniki ili waweze kupewa vidonge vya folic acid pamoja na vidonge vya malaria ambavyo wasipomeza wanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na changamoto hiyo.
“Idadi kubwa ya watoto ambao tunawapokea kituoni hapa wengi wanatoka Tabora,Bihalamuro,Kigoma na Musoma na idadi kubwa zaidi ni Mwanza kwa sababu huku changamoto iliopo tunapokea wazazi wengi ambao hawana uwezo wa kuwahudumia hao watoto wengi wao ni wanawake wakiwa wametelekezwa,”.
Pia anaeleza kuwa mbali na changamoto hiyo pia watoto wengi wanaowapokea wanakabiliwa na utapia mlo ambao unachangiwa na lishe duni ambapo kama shirika wanawasaidia katika vipimo na matibabu huku serikali kupitia hospitali hiyo ikisaidia huduma ya upasuaji bure.
“Tulianzisha kituo hiki mwaka 2017 ambapo kwa wiki kituo kinapokea watu 60 ikiwemo wazazi na watoto wao huku kwa mwaka ni takribani watoto 600, ambapo idadi ya watoto imeongezeka sana kuanzia mwaka jana hii ni kutokana na elimu tulioitoa hivyo mama akizaa mtoto mwenye matatizo hayo hamfichi,” ameeleza Getruda.
KAULI YA MTAALAM WA AFYA
Naye Daktari wa Upasuaji wa ubongo na mgongo hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,Dkt. Gerald Mayaya, anaeleza kuwa ugonjwa wa kichwa kikubwa ni ugonjwa wa kujaa maji kichwani kuliko kawaida.
Je? ni nani anaweza kupata ugonjwa wa kichwa kikubwa
Dkt. Gerald anaeleza kuwa ugonjwa wa kichwa kikubwa unaweza kumpa mtu yoyote lakini akipata mtoto kichwa kinakuwa kikubwa huku mtu mzima akipata akiongezeki kinabaki vilevile.
SABABU YA KICHWA KUONGEZEKA
Anaeleza kuwa kwa sababu mifupa ya kichwani ipo nane na mtoto akiwa mdogo mifupa yote inakuwa bado haijafunga akipata shida katika kichwa kinakuwa kikubwa kwani inakuwa bado haijakomaa na kuungana lakini mtu mzima kichwa kinakuwa tayari kimeisha unga na ndio maana dalili zinakuwa tofauti za ugonjwa huo.
Anafafanua kuwa akipata mtoto mdogo maana yake maji yanajaa kule ndani ya ubongo ambapo kila mwanadamu ana maji kwenye ubongo na kila mwanadamu anazalisha maji kati ya mililita 400 mpaka 500 kwa saa 24.
“Kinachotokea maji kujaa kuliko kawaida kwenye ubongo,katika hali ya kawaida ni kuwa kile kiasi kinachozalishwa cha mililita 400 hadi 500 ni kiasi cha mililita 100 hadi 150 pekee,kinabaki katika mzunguko wa kawaida wa ubongo na uti wa mgongo na kazi yake ni kulinda uti wa mgongo na ubongo,” anaeleza Dkt.Gerald na kuongeza kuwa
“Kiasi cha mililita 350 kinachobaki kinarudishwa katika mfumo wa damu na yananyonywa kule ndani na ili mtu apate maji kupita kiasi ni aidha uzalishaji wa maji ni mwingi zaidi kuliko kile ambacho kinarudishwa kwenye mfumo wa damu ama kwenye njia za kupitisha maji ziwe zimeziba maana yake mtu anaweza kupata shida ya kichwa kujaa maji kuliko kawaida,”.
Nini kinasababisha ubongo kujaa maji(kichwa kikubwa
.
Dkt.Gerald anaeleza kuwa visababishi ni viwili maji yanazalishwa kwa wingi zaidi au njia zimeziba hivyo hayawezi kufika mwisho kama vile maji ya mto ukiyaziba yatatafuta njia ya kwenda maeneo mbalimbali.
Anaeleza kuwa maji yakizalishwa kupita kawaida au njia kuziba zile njia zake zinatanuka na kwa sababu njia hizo zipo katikati ya ubongo maana yake ubongo ndio unaendelea kuumia watoto wadogo vichwa vinakuwa vikubwa lakini kwa watu wazima yeye anapata maumivu ya kichwa sana pamoja na macho kutooana vizuri, kutapika na inaweza kupelekea upofu.
“Tunawastani wa kuwafanyia watu wazima kila mwezi angalau mtu mmoja au wawili wenye shida hiyo kwa watoto tunawafanyia upasuaji kwa wastani kwa wiki watoto 10 hadi 15 na kwa mwaka ni wastani wa watoto 200 hadi 300 na kwa ulimwengu mzima changamoto hii ni kati ya kila vizazi 1000 ni watoto kati ya 1 mpaka 3,wanakuwa na shida ya kichwa kikubwa,”.
Je?mgongo wazi ni nini
Anaeleza kuwa ugonjwa wa mgongo wazi ni mfumo wa fahamu ambao umegawanyika kati ya ubongo na uti wa mgongo kwenye mfumo huo wa uti wa mgongo mpaka juu kichwani mtoto anaweza kuzaliwa na kivimbe chochote.
“Kwa asilimia kubwa tunapata watoto waliothiriwa uti wa mgongo kwa chini kinachotokea wakati mtoto akiwa anatengenezwa ndani ya zile siku 30 ndio wakati uti wa mgongo unafunga,mtoto kuzaliwa na mgongo wazi au kichwa kikubwa maana yake ule mfumo wa fahamu ukichelewa kufunga ndani ya siku hizo ndio hali hiyo inatokea,”anaeleza.
Ambapo kwa kawaida uti wa mgongo unafunikwa na mifupa kisha kava ambazo zipo tatu baada ya hapo ndio unapata uti wa mgongo ndani hivyo vyote ni kwa ajili ya kulinda uti wa mgongo ambao ni kiungo muhimu sana katika mwili wa binadamu.
Kinachotokea siku 25 za kwanza kunaweza kutokea uti wa mgongo juu au chini kusifunge ndio sababu ya kuzaliwa na madhara ambapo utakuta mtoto katika eneo hilo amezaliwa bila mifupa au mifupa haijafunga na zile kava za kwenye uti wa mgongo unakuta zimenyanyuliwa na maji.
“Mfumo wa fahamu unazungukwa na maji kwaio msukumo “presha” ya maji itasukuma na kupeleka eneo ambalo halina mfupa yakiisha jitokeza sehemu hiyo inatokea mtu kuzaliwa na uvimbe kwenye uti wa mgongo hiyo baada ya siku 25 za mwanzo za ujauzito,”.
Nini sababu ya watoto kupata changamoto hiyo
Anaeleza kuwa kuna baadhi ya tafiti zinaeleza na kuonesha kuwa upungufu wa folic acid unachangia tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi ambapo watoto wenye mgongo wazi kabla na baada ya kufanyiwa upasuaji asilimia 60 hadi 80 ya watoto hao wana”pata pia shida ya kichwa kikubwa.
“Ndio maana wanashauri kuwa mama akiwa mjamzito anaweza akawa anameza kidonge kimoja cha folic acid hususani siku za mwanzo za ujauzito au kama mtu anatarajia kupata mimba ameze vidonge hivyo mpaka atakapopata ujauzito kwani shida inatoke zile siku 26 hadi 30 za mwanzo wa mimba ingawa changamoto wengi wanakuja kujigundua kuwa wana ujauzito muda ukiwa umepita,”anaeleza.
Sanjari na hayo anaeleza kuwa ugonjwa wa kichwa kikubwa umegawanyika katika sehemu kuu mbili kuna sababu ya kuzaliwa na kuna sababu ya mtoto kupata baada ya kuzaliwa.
Sababu za kuzaliwa
Anaeleza kuwa sababu ya kuzaliwa ni pamoja na njia inayotumika kupitisha maji kuwa ndogo au watoto wanaozaliwa wakiwa njiti(wanaozaliwa kabla ya siku) kuna wakati wanavuja damu kwenye ubongo au mama anaweza kuwa na maambukizi ya maradhi wakati wa ujauzito hivyo kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na changanamoto hiyo.
“Ndio maana mama akienda kliniki kwa mara ya kwanza wanampima ili kujua kama ana maradhi mbalimbali ambayo pia baadhi ya watoto uzaliwa na matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa kutokana na kuzaliwa wakiwa hawana sehemu katika ubongo ambazo utumika kufyonza maji maana yake maji yanazalishwa hila hayawezi kufika mwisho,”
sababu za baada ya mtoto kuzaliwa
Daktari huyo anaeleza kuwa sababu ya baada ya kuzaliwa ni pamoja na mtu anaweza kupata ajali kisha damu ikavujia kwenye ubongo na ndio maana wanasema mtu mzima anapata changamoto ya kichwa kujaa maji kuliko kawaida au maambikizi mfano uti wa mgongo.
Hivyo kutokana na hali hiyo zile sehemu ambazo zinatumika kufyonza maji na kurejesha katika mfumo wa damu zitashindwa kufanya kazi na maji yatazalishwa lakini zile sehemu unakuta zinakuwa na makovu au haziwezi kufanya kazi vizuri.
“Kwa ajali kutokea na damu kuvujia kwenye ubongo,uti wa mgongo kupata matatizo au mtu kuwa na uvimbe kwenye ubongo mara nyingi tunapata kesi hizi kwa watoto ambao wana miaka 2 hadi 10 kisha anapata shida ya kuwa na kichwa kikubwa vilevile kwa watu wazima pia,”anaeleza.
Nini kifanyike kupunguza changamoto hiyo
Anaeleza kuwa katika kuhakikisha wanapunguza watoto kuzaliwa na changamoto hizo anashauri wanawake kula chakula,matunda na mbogamboga zenye folic acid ni kitu kizuri kwa sababu ukiangali shida hii mara nyingi inawapata watu walio na maisha ya chini ukilinganisha na wenye uwezo ambapo anaeleza kuwa wakipungua watoto wenye mgongo wazi moja kwa moja wa vichwa vikubwa nao watapungua.
Azungumza sababu ya pacha kupata changamoto hiyo baada ya kuzaliwa
Akizungumzia hali ya mapacha ambao walizaliwa vizuri ila baada ya muda mmoja akapata maambukizi Daktari huyo anaeleza kuwa sababu ni kuwa vinasaba(genetic),ambapo kwa kipindi cha miaka minne imeisha tokea mara mbili kwa pacha mmoja kuzaliwa na kichwa kikubwa na baada ya miezi minne pacha mwingine akapata ugonjwa huo.
Ambapo anaeleza kuwa tafiti ambazo zimeisha fanywa zinaonesha asilimia 4 pacha wa kwanza akizaliwa na kichwa kikubwa kuna uwezekano wa pacha mwingine akapata ugonjwa huo.
Licha ya kuwa kilichosababisha mtoto wa kwanza kuzaliwa na kichwa kikubwa ni tofauti na pacha wa pili,unaweza kukuta maji yanazalishwa vizuri lakini hayafyonzwi vizuri huyo wa kwanza lakini huyo mwingine unakuta alipatwa na uvimbe kwenye ubongo au maambukizi.
Hata hivyo akizungumzia hali ya pacha mmoja kupata ugonjwa wa kichwa kikubwa baada ya kuzaliwa huku mwenzie akiwa kawaida Daktari huyo anaeleza kuwa kama pacha mmoja kabla ya kupata kichwa kikubwa alichemka sana maana yake alipata maambukizi na haihusiani kuwa mwenzie naye anaweza kupata.
“Kila siku tunapokea wastani wa mtoto mmoja mpaka wawili maana yake ni pamoja na wale ambao wameisha fanyiwa upasuaji na amepata shida nyingine,zamani tulikuwa tunapata watoto wenye changamoto hiyo ambao wameisha kuwa wakubwa lakini kwa sasa ukipita wodini kwetu unakuta watoto waliochini ya umri wa miezi 6,hii inaonesha watu wamepata elimu na uelewa juu ya suala hili na wamejua umuhimu wa kuwawaisha mapema hospitali,”.
Je?watoto wenye kichwa kikubwa wanaweza kupona
Anaeleza kuwa mtoto mwenye tatizo la kichwa kujaa maji kupita kawaida akitibia kwa wakati kabla ubongo haujaathirika sana anaweza akapona na kuendelea kufanya shughili zake kama kawaida.
“Tunao ushahidi wa baadhi ya watoto ambao tuliwatibu hapa na sasa wapo shuleni wanafanya vizuri katika masomo,akifanyiwa upasuaji mapema kuna uwezekano wa kupona kichwa kikubwa na mgongo wazi vilevile,”.
Aidha anaeleza kuwa changamoto ni jamii kuwa na imani potofu huku wanaume wakiwambia watoto na kuwaachia mama zao wakiamini kuwa ni mikosi.
“Kesi kama hizo ameisha kutana nazo mara nyungi ambapo mara ya kwanza kumleta mtoto hospitali unakuta analetwa na baba na mama ila mara ya pili analetwa na mama pekee uzuri akirudi mtoto akitibiwa na kuwa vizuri baada ya miezi mitatu unakuta wanarudi wote.
Nini hatua za kuchukua
Anaeleza kuwa kimsingi mtoto akizaliwa akawa na dalili za kichwa kikubwa au mgongo wazi wanatakiwa kuwaishwa hospitali kwani kuna njia mbili za upasuaji moja ikiwa ni ya kuingiza mpira.
Na ya pili kama njia ya maji imeziba wanamfanyia upasuaji kwa ajili ya kutafuta njia nyingine ya kupitisha maji ili yaendelea kushuka kama kawaida na njia hiyo ni nzuri kama kila kitu kitakuwa sawa anaweza hata asirudi hospitali.
Gharama za matibabu ya magonjwa hayo
Gharama za matibabu kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano wenye changamoto hiyo katika hospitali hiyo ni bure isipokuwa kuna wale watoto unakuta gharama halisi mpira tu unagharimu kiasi cha shilingi laki tatu lakini mpira unatolewa bure.
Anazungumzi gharama halisi ambayo inapaswa kulipwa kwa ajili ya matibabu hayo kwa watoto hao endapo kama serikali isinge saidia ambapo serikali na hospitali umejitahidi kuhakikisha vitu vinaendelea ingawa watoto hawachangii chochote.
“Tukifanya upasuaji ambao siyo wa kuweka mpira tunatumia kifaa mabacho kinagharimu kiasi cha millioni 300 hadi 400,hivyo tukisema kama ni kulipia mtu anaweza kulipa wastani wa milioni 1 hadi milioni 1.5,inagawa matibabu yote yanatolewa bure chini ya umri wa miaka mitano,”.
Anaeleza kuwa gharama ambayo mzazi anapaswa kuchangia ni kiasi ambacho hakizi 50,000 kwa ajili ya vipimo vya msingi.
“Gharama za mtoto mmoja kama angekuwa analipia wa kichwa kujaa maji kuliko kawaida ni kubwa sana ambapo kuna watoto wanaa bahati mbaya unakuta anawekewa mpira zaidi ya mara tano na gharama yake mmoja ni 300000, mpira huo kama ana shida yoyote anawekewa mara moja,”.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika