Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amewataka wataalam wa afya wilayani humo kuendelea kuwaibua watoto wenye utapiamlo mkali ili waweze kupatiwa matibabu.
Munkunda ametoa kauli hiyo leo wakati akifunga kikao cha kujadili utekelezaji wa maazimio ya mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 pamoja na taarifa ya lishe kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2020 .
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wilaya inapunguza kama siyo kumaliza kabisa tatizo la utapiamlo. Aidha amesema ili jamii iweze kushiriki vema katika shughuli mbalimbali za maendeleo ni lazima iwe na afya njema ambayo hupatikana kwa mtu kuwa na lishe bora.
Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo kuwapongeza wataalam wa afya wanaotoa huduma vituoni na watoa huduma ngazi ya jamii kwa kushirikiana vema na Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) kupitia mradi wa lishe endelevu, wameweza kutekeleza afua tisa za mkataba huo kwa asilimia 81.7 katika kipindi hicho.
Munkunda amesema kuwa hata shule zitakapofunguliwa Juni 29 mwaka huu wilaya imeweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni ili waweze kumudu vizuri masomo yao.
Ametoa wito kwa akina mama wajawazito kutumia vidonge vya kuongeza damu lakini pia wataalam wa afya waendelee kutoa unasihi wa lishe kwa wazazi au walezi wa watoto wenye umri kati ya miezi 0 hadi miezi 23 huku akiwasihi kuèndelea kutoa matone ya Vitamini ‘A’ kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Dkt. Philipina Philipo ameushukuru uongozi wa Jukwaa la Lishe kwa kushirikiana vema na Wilaya ya Bahi kutekeleza maazimio ya mkataba wa lishe.
Naye Mkurugenzi wa Mtendaji wa PANITA, Tumaini Mikindo ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kutekeleza maazimio hayo na ameiomba halmashauri kuendelea kufanya ukaguzi wa vyakula katika maeneo ya biashara na kutoa fedha kupitia mapato ya ndani kutekeleza shughuli za lishe.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba