January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online,Dar

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Ally Hamisi, amesema jamii ishirikiane na taasisi mbalimbali za kusaidia na kuwalea watoto wenye uhitaji.

Akizungumza Januari 9,2025,katika hafla ya utoaji wa msaada wa vifaa vya shule ikiwemo sare za shule,mabegi,viatu pamoja na madaftari vilivyotolewa na taasisi ya Lalji Foundation kwa watoto yatima,Mwanaidi amesema,suala la malezi kwa watoto wenye uhitaji,linatakiwa kushirikiana kwa pamoja.

“Makundi hayo yanahitaji usaidizi wetu,na wao wapate huduma stahili ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha,”.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya Lalji Foundation,Imtiaz Lalji,amesema kutoa msaada kwa watoto yatima ni jambo la baraka na kizalendo,ambapo taasisi imetoa msaada kwa wanafunzi wa vituo 9, vya kuelekea watoto,huku akisisitiza kuwa imekuwa ni utaratibu wa taasisi hiyo kusaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Nae Katibu wa taasisi hiyo,Fatema Lalji amesema taasisi hiyo,inashughulika kusaidia watu wenye mahitaji maalumu katika  sekta ya uchumi, afya, elimu, watoto yatima na masuala ya kijamii.

“Taasisi ya Lalji Foundation imefanikiwa kufanya kambi ya macho katika maeneo tofauti tofauti katika wilaya ya Kahama, Geita, Songea, Kigoma na Dar,pia imesaidia watoto wenye ulemavu wa viungo kwa kuwapatia viungo bandia katika hospital CCBRT Mkoa wa Dar es salaam,”.