November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana na kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa waruhusiwa

-Muhimbili yaishukuru awamu ya sita kutokana na uwekezaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na uwekezaji uliofanyika hospitalini hapa ambao umewezesha huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi kufanyika ikiwemo upasuaji mkubwa wa kutenganisha watoto pacha.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuwaruhusu watoto pacha waliozaliwa kwa nje wakiwa wameungana tumbo na kifua, ndani waliungana ini na mfupa wa kidari, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi, amesema uwekezaji wa kusomesha watalaam, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi vya kisasa umeiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma zinazolingana na hadhi yake.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Dkt. Victor Ngota ameeleza kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao, ulichukua saa sita na kuhusisha jopo la wazawa lenye utaalam mchanganyiko wa hali ya juu wa madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, usingizi na ganzi, watalaam wa lishe pamoja na radiolojia.

“Tuliwapokea watoto hawa tarehe 11 Machi 2023 wakiwa na jumla ya kilo nne hivyo tulianza mchakato wa kuwahusisha wataalam ambao wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha ili kuweza kupata dira ya namna watakavyoishi mara baada ya kutenganishwa ambapo hadi wanatenganishwa walikua na kilo 16 sawa na kilo nane kwa kila mmoja” amefafanua Dkt. Ngota.

Mzazi wa watoto hawa Mariam Shabani, mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam, ameishukuru Serikali na watoa huduma wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi alivyohudumiwa katika kipindi chote alichokuwa hapo.