Na Suleiman AbeidTimesmajira Online, Shinyanga
MRATIBU wa chanjo mkoani Shinyanga, Timothy Sosoma ametoa wito kwa wazazi wote wa mkoa huo wenye watoto ambao hawajakamilisha chanjo ya pili na ambao hawajapata chanjo kabisa kuwapeleka vituoni watoto wao ili waweze kupatiwa chanjo.
Sosoma anatoa wito huo wakati akitoa taarifa ya hali halisi ya zoezi la chanjo mkoani Shinyanga ambapo amesema mpaka hivi sasa mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kuchanja asilimia 58 ya watoto wote waliotarajiwa kuchanjwa.
Anasema mpaka hivi sasa Mkoa wa Shinyanga unaendelea na utekelezaji wa zoezi la kuwatafuta watoto ambao hawajakamilisha chanjo walengwa ni wale waliopatiwa chanjo tangu mwaka 2019 hadi 2022 na ambao hawajarudi tena kuchanjwa.
Anasema katika utafiti ambao wameufanya wamebaini kuwa Mkoa wa Shinyanga una watoto wapatao 97,138 wanaotakiwa kupatiwa chanjo kwa ajili ya kinga ya ugonjwa wa surua na kwamba zoezi hilo limeanza kutekelezwa tangu Machi 23 na litaendelea hadi Machi 29, 2023.
Hadi Machi 26, 2023 ikiwa ni siku ya nne wameweza kufikia watoto 56,289 sawa na asilimia 58 kiwango ambacho bado hakijaridhisha ila wanaamini kwa siku mbili zilizobaki wataweza kufikia lengo la watoto wote waliolenga kuwafikia.
“Tunafanya hivi kuwatafuta hawa watoto ili waweze kukamilisha chanjo zao ili kuepukana na milipuko inayotokea katika sehemu mbalimbali za nchi yetu, watoto wanatakiwa wapate chanjo kamili ili wawe na kinga kamili dhidi ya magonjwa yanayolengwa kuwakinga,” anaeleza Sosoma.
Sosoma anafafanua kuwa mpaka sasa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu ndiyo ipo nyuma katika zoezi zima la chanjo ambapo hadi kufikia Machi 26, 2023 ilikuwa imechanja asilimia 30 kati ya lengo lililowekwa.
“Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ambayo mpaka sasa ndiyo inayoongoza baada ya kuwa imechanja asilimia 99 ikiwa watoto waliochanjwa ni 160,518 na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imechanja watoto 12,431 sawa na asilimia 67,”na kuongeza kuwa
“Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga 10,375 ikiwa ni asilimia 58, Manispaa ya Shinyanga imechanja watoto 2,665 sawa na asilimia 45 na Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama imechanja watoto 9,567 sawa na asilimia 45,” anaeleza Sosoma na kwamba takwimu hizo ni kwa chanjo za kinga ya surua.
Katika hatua nyingine Sosoma anatoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano anayestahili kupatiwa chanjo awe amepata chanjo na kama bado basi wapelekwe vituoni ili wapatiwe chanjo hiyo ili kuwakinga na magonjwa ya milipuko.
Anasema hivi sasa zoezi linaloendelea ni kutoa chanjo zote lakini kipaumbele ni kwa chanjo ya kinga ya surua kutokana na baadhi ya maeneo hapa nchini kuripotiwa kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa surua hivyo juhudi zinachukuliwa kuhakikisha kila mtoto anapatiwa chanjo.
“Kwa mkoa wa Shinyanga hatujapata mlipuko wa surua, na iwapo itatokea taarifa zitatolewa mara moja kwa wananchi, lazima tuwajulishe, kwa sasa hatua ugonjwa huo, tunaendelea kuchukua sampuli pindi inapotokea mtoto kuonekana na vipele na homa tunapeleka kwa ajili ya vipimo kuthibitisha kama ni surua, lakini hatua ugonjwa huo,” anaeleza.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria