Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online, Tanga
Watoto nane wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa baada ya kurubuniwa kwenye kibanda cha mihogo kilichopo karibu na shule yao katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amelaani kitendo hicho na kuagiza kufanyika kwa kura za siri ili kubaini watu wote wanaounga mkono vitendo hivyo wilayani humo.
Balozi Dkt Burian amesema kitendo cha aina hiyo pia kimeripotiwa katika Wilaya ya Mkinga na kuitaka jamii kufunga kibwebwe kupambana na vitendo hivyo ambavyo vikiachwa vinaweza kuathiri vizazi vya sasa na vya baadae.
Mkuu wa Mkoa Dkt.Batilda ametoa maagizo hayo Juni 21,2024 wakati akiwa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kupokea taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo Halmashauri hizo zilipata hati safi.
Balozi Dkt Burian amesema kuwa iwapo uchunguzi utafanyika na akapatikana mtu yeyote awe Mwalimu au Kiongozi wa dini yeyote hawatamuacha kwani vitendo hivyo vimekuwa vikidhoofisha nguvu kazi ya Taifa.
“Watu wazima wameanzisha kigenge cha makusudi cha danganya toto,kumbe wana shughuli zao nyingine watoto wakienda wanadanganywa na mihogo ya kukaanga,wanawadhulumu watoto wadogo wa kike wa miaka 8, 9 mpaka 10 huyo wa mwisho alienda akapatwa na changamoto ya kutokwa na damu nyingi kwa kuwa alikuwa ni mdogo ndio watu wakajua,”ameeleza Balozi Dkt Batilda na kuongeza kuwa
“Nauliza jamani Handeni hili suala halijawachukiza mmekaa kimya nilifikiri mtaenda pale kwa hasira mkiwa mmefunga vibwebwe watoto wamefanyiwa ukatili au mnataka watu wa Mwanza ndio waje na vibwebwe na maandamano kuwasemea nyinyi watu wa Handeni?,”.
Pia ameeleza kuwa jambo kama hilo amelikuta Mkinga p mtoto wa miaka mitatu wa kike amebakwa na kulawitiwa huku akihoji kuwa “hivi huyo mtoto amekosa nini na ana dhambi gani?.
Hata hivyo amesisitiza kuwa jambo hilo watalishughulikia ambapo wanasheria wanaisimamia hiyo kesi lazima hukumu ipatikane na iwe fundisho.
“Tutaanza kura za siri kutaja walawiti, wabakaji wa watoto wa kike na wa kiume shuleni huko ipite kura ya siri na wataalamu wanajua nani anaonewa na anayefanya kweli,tushirikiane tukikaa kimya hata sisi tutakuwa hatujawatendea haki wanahandeni,” Balozi Dkt Batilda.
Aidha amefafanua kwamba endapo mtoto ataingiliwa kinyume na maumbile atakuwa amepoteza sifa ya kujiunga na majeshi yote nchini jambo ambalo linapaswa kupigwa vita ili kuweza kupata makomando watakaokwenda kupigana maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Handeni Mussa Mkombati amekiri kuwepo kwa suala hilo na kueleza kuwa wanalishughulikia ipasavyo hadi kufikia kutoa ahadi ya zawadi kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa mtu anayehusika na ubakaji na ulawiti.
“Tunapofanikiwa kumkamata mbakaji au mlawiti tunakosa ushirikiano kutoka kwa jamii kwa maana suala likishakuwa polisi na kutakiwa kwenda mahakamani,jamii husika wanalitoa suala hilo nje ya sheria na kulipeleka nyumbani jambo ambalo linatukwamisha katika mapambano yetu, “amesisitiza Mkombati.
“Bado hatujakata tamaa tunaendelea kupambana kuhakikisha waliohusika na matukio haya sheria inachukua mkondo wake na wanapata adhabu stahiki ikiwa ni pamoja na kuendelea kupambana na wabakaji na walawiti kwa kuunda kamati za kuchunguza wanaotekeleza vitendo hivyo nje na ndani katika shule zote za wilaya hiyo,”.
Tukio la wanafunzi wanane kubakwa na kulawitiwa Wilayani Handeni Mkoani Tanga lilifanyika mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu ambapo walibaini matendo hayo baada ya binti wa miaka 8 aliyebakwa kwa mara ya mwisho kupata changamoto ya damu na kuwataja wenzake waliokuwa wakifanyiwa vitendo hivyo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato