Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Ili kuwa na jamii inayozingatia lishe bora na kuepusha vifo vya watoto,Watendaji wa Kata na Mitaa wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha masuala ya lishe kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa kuhakikisha wanawahimiza wahudumu ngazi ya jamii kuwaibua watoto waliopo mitaani na kuwapeleka katika vituo vya huduma za afya ili kupata huduma bora na kuepusha vifo vya watoto.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Masala katika kikao cha tathmini ya lishe Wilaya ya Ilemela chenye lengo la kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022-2023.
“Kuweni mstari wa mbele katika suala la lishe ili kuhakikisha tunakuwa na jamii inayozingatia lishe bora,” amesema Msengi.
Katika kikao hicho wajumbe walipitia taarifa ya kadi alama ya lishe ya mwaka 2022/2023 ambayo ilionekana kupanda ukilinganisha na mwaka 2021/2022 ambapo viashiria vingi vikiwa na asilimia kati ya 70-100 hivyo kuwa katika rangi za kijani na njano ambapo rangi ya kijani inawakilisha vizuri na njano ikiwakilisha wastani.
Pamoja na mafanikio hayo yaliyobainishwa katika kadi alama ya lishe zipo changamoto mbalimbali zilizobainishwa ikiwemo suala la ushiriki mdogo wa wanaume katika mafunzo ya jiko darasa.
Ambapo Watendaji wa Kata na Mitaa wametakiwa kuwaelimisha wanaume juu ya umuhimu wao katika kushiriki kwenye mafunzo hayo mara yanapotolewa katika mitaa yao ili kuweza kuimarisha afya za watoto kwani wanaume wengi ndio wanaotoa fedha za manunuzi ya chakula.
Kadhalika wajumbe walipata fursa ya kujadili juu ya zoezi la siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIKI) ambayo inalenga kuimarisha mifumo ya kijamii ya utoaji na usambazaji wa huduma endelevu za afya na lishe ya mama, mtoto na jamii kwa ujumla.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua