November 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji wa vijiji na kata kusimamia rasilimali za uvuvi

‎Na Israel Mwaisaka, Rukwa

‎VIONGOZI  wa  vijiji na kata wanalo jukumu kubwa la usimamizi wa rasilimali za uvuvi endapo watawashirikisha wadau wote wa uvuvi katika kuhakikisha rasilimali hiyo inatunzwa na kuleta manufaa kwa jamii.

‎Hayo yamesemwa na mwakilishi wa mkurugenzi wa uvuvi Bugomba Kimasa ambaye pia ni afisa uvuvi mkuu alipokuwa akifunga Warsha ya siku mbili kwa maafisa uvuvi,wawakilishi  wa BMU , maafisa watendaji wa jiji na kata,wenyeviti wa vijiji na BMU mtandao iliyoandaliwa na taasisi ya The Nature Conservancy katika kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa.

‎Alisema kuwa  wadau wote wakijenga mahusiano na kushirikiana kwa ukaribu itawezesha kukabiliana na uvuvi haramu   hasa ule unaoharibu mazalia ya samaki kitu ambacho Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wanalipa kipaumbele.


‎Kimasa alidai kuwa katika mapambano ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi Wananchi ni moja ya nguzo muhimu katika kuyafikia malengo waliyoyaweka hivyo ni muhimu kushirikishwa katika hatua zote muhimu za ulinzi wa rasilimali hizo za uvuvi.

‎Mkuu wa divisheni ya mifugo na uvuvi wilayani Nkasi Dkt,Johnshauri Tlatla kwa upande wake alishauri kuwepo kwa faini kubwa kwa  Wavuvi haramu na kuwa hiyo ndiyo itakuwa ni suluhisho la tatizo hilo.

‎Alidai kuwa kwa kuwa katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi jamii imepewa jukumu la kutengeneza Sheria ndogo amedai upo umuhimu mkubwa wa kutunga Sheria ngumu zitakazokuwa na maumivu na kuwa hilo ndilo litakua ni suluhisho la ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

‎Dkt.Tlatla alifafanua kuwa kwa mfano katika ziwa Tanganyika yapo maeneo tengefu yaliyotengwa ili yasiingiliwe na Wavuvi lakini wapo wanaokiuka Sheria ya ulinzi wa maeneo hayo tengefu kwa makusudi wakati wanafahamu kabisa kuwa kufanya hivyo nikuharibu mazalia ya samaki lakini pia wanavunja Sheria na kuwa suluhisho lake ni kuwepo kwa Sheria Kali dhidi ya wahalifu wa namna hiyo.

‎Washiriki wa warsha hiyo kwa pamoja walikubaliana baadhi ya mambo muhimu ikiwemo utengenezaji wa chombo kimoja cha usimamizi na uongozi utakavyokua ikiwemo na Sheria moja itakayotafsiri shughuli za uvuvi.

‎

‎

‎