March 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji wa uboreshaji Tanga, Pwani watakiwa kufuata sheria kuhamasisha wananchi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Onlinmr

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa ya Tanga na Pwani kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Asina Omari wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA Mkoani Pwani Februari 03,mwaka huu.

“Mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zilizotungwa chini ya vipengele vya sheria hiyo vinavyohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”amesema Jaji Asina.

Aidha, ametoa wito kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanaendelea kutumia muda wao wa ziada kusoma na kupitia maelekezo yote waliyopewa ili kuongeza uelewa zaidi kuhusu wajibu na majukumu yao katika zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mwenyekiti wa Mafunzo kutoka Mkoa wa Tanga, Mwanaidi Nondo akizungumza jambo kuhusiana na mafunzo hayo waliyopewa.

“Ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani,” amesema Jaji Asina.

Akifunga mafunzo kama hayo Mkoani Tanga na kuhusisha washiriki kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe, Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Magdalena Rwebangira amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.

“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” amesema Rwebangira.

Amesisitiza kuwa, jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji, kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo mlizo nazo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akiwa katika ufungaji wa mafunzo hayo mkoani Tanga.

“Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika shehia zote zilizopo katika mikoa yote mitatu ya Unguja. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika shehia zote,” amesema Magdalena.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Tanga na Pwani umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025 ambapo vituo vitafunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Kailima R.K akizungumza jambo na washiriki mkoani Tanga. 
Washiriki wa Mafunzo kutika Mkoa wa Pwani wakiwa katika ufungaji wa mafunzo.
Washiriki wakifanya mazoezi kwa vitendo kwa kuandikisha wapiga Kura wapya, kuboresha taarifa  na kufuta waliopoteza sifa.