January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji Songwe wapatiwa mafunzo uboreshaji daftari la mpiga kura

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa mafunzo ya uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa watendaji ngazi ya Mkoa wa Songwe na
Kuwataka kutumia elimu na ujuzi watakaoupata kwenye mafunzo hayo kuwezesha zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi.

Akifungua mafunzo hayo Leo Januari Mosi, 2025, Mkurugenzi wa Idara ya usimamizi wa uchaguzi kutoka tume hiyo, Grayson Orcado, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa,Jacobs Mwambegele, amesema watendaji hao wanapaswa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ikiwemo kutumia elimu watakayopata kwenye mafunzo hayo ya siku mbili ili kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi.

“Ni matarajio ya tume kuwa, kutokana na semina hii kila mmoja wenu atapata elimu na ujuzi wa kutosha utakaomuwezesha kutekeleza majukumu yake ili kuboresha daftari” alisema Orcado akisoma hotuba ya Mwenyekiti wa tume Jaji Mwambegele.

Hotuba hiyo ya Jaji,Mwambegele, ilibaisha kuwa mafunzo hayo pia  yamelenga kuwajengea umahili watendaji hao wa ngazi ya mkoa ili kuwawezesha nao kwenda
kuwafundisha wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata ambao nao wataenda kutoa mafunzo hayo kwa wasimizi katika ngazi za vituo.

Vile vile, hotuba hiyo imeeleza kuwa, wakati wa uboreshaji daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikishia  wapiga kura kwa kuwa jambo hilo ni muhimu na litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima, lakini pia mawakala hao watasaidia kuwatambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizo za lazima.

“Pamoja na kuruhusiwa kuwepo vituoni lakini  mawakala hawa wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura kituoni”.

Tayari Tume ya Taifa ya Chaguzi imetangaza ratiba ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura kwenye mikoa ya Rukwa, Njombe, Songwe na Ruvuma ambapo zoezi hilo l litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 hadi 18 Januari, 2025.

Kwa mujibu wa Tume mikoa hiyo itafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa tisa na kwamba tayari Tume imekamilisha uboreshaji kwenye mikoa 19 ambayo ilijumuisha mizunguko nane kati ya mizunguko 13 ambayo imepangwa kukabilisha zoezi hilo nchini. 

Mikoa ambayo tayari imekamisha zoezi hilo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida. 

“Mikoa mingine ni mikoa ya Zanzibar ambayo ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha na Kilimanjaro. Kwa sasa mikoa miwili ya Mbeya na Iringa inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 02 Januari, 2025,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.