Na David John,TimesMajira,Online, Dar
KAMPUNI ya Puma Energy Limited imeahidi kuendelea kuhakikisha ubora wa hali ya juu wa mafuta unazingatiwa kuanzia yanapohifadhiwa hadi yanapoingia kwenye chombo cha usafiri cha wateja wao.
Ahadi hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy Limited, Dominic Dhanah, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja wa kampuni hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Amesema wanajivunia uwezo na sifa yao na watailinda kwa wivu mkubwa kuhakikisha wateja wao wanapata huduma mbalimbali katika vituo vyao vya mafuta kote nchini.
“Wiki hii ni muhimu sana kwetu kama kampuni ya mafuta kwa kuwa inatupa fursa ya kukutana na wadau wetu katika biashara za uuzaji wa mafuta vituoni ikiwemo wamiliki wa maduka katika vituo vyetu.
Pia tunakutana na waendeshaji wa vituo hivyo na kwa namna ya pekee kabisa wateja wetu ndio roho na moyo wa kampuni yetu,”amesema Dhanah na kuongeza;
“Sisi kama Kampuni kwa upande moja na wadau wetu kwa upande mwingine tunapata fursa ya kujadiliana na kupata maoni yao juu ya mambo muhimu kama umuhimu wa mteja katika biashara yetu.
Ubora wa bidhaa na huduma zetu vituoni, usalama na afya eneo la kituo.”
Amesema lengo lao ni kuwawezesha kupata mrejesho sahihi utakao wawezesha kuweka misingi imara ya ubora wa huduma zao na zaidi kuwatambua wale wanaofanya vizuri na zaidi miongoni mwao kuwashukuru kwa utendaji wao nzuri.
Amefafanua kuwa mkakati wao kama Puma Energy ni kumuweka mteja katikati ya kila wanalofanya kama kampuni.
“Mteja ndiye mtu mmoja pekee na wa muhimu sana katika biashara yetu na lengo kuu la kuadhimisha wiki hii ni kuhakikisha kwamba wateja na wadau wao wote wanakumbushwa kwamba kampuni yao inawajali na kuwathamini sana,” amesema.
Dhanah amesema maadhimisho ya mwaka huu yanatokana na mafanikio makubwa ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja yaliyofayika katika vituo vyote vya mafuta vya kampuni ya Puma duniani Desemba, Mwaka 2019.
Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika vituo vyote vya mafuta vya Kampuni ya Puma duniani na kwa hapa Tanzania wataadhimisha katika mikoa yote nchini ambako Puma inafanya biashara ya vituo vya mafuta kuanzia Novemba 30,2020 mpaka Desemba 2020.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakari Kunenge aliipongeza Puma Energy kwa huduma bora wanayoitoa kwa Watanzania, huku akitumia fursa hiyo kutoa maagizo kwa kampuni za mafuta nchini kuzingatia matakwa ya kisheria ya leseni zao pindi wanapotoa huduma hiyo.
Pia amewataka kuzingatia ubora ,usalaman na misingi halali ya kufanya biashara zao sokoni na kwamba waendelee kuangalia wafanyakazi wao, kwani wao ndiyo wanaifanya kuwa bora ndani ya kampuni hiyo ya mafuta.
Kunenge alitoa kauli hiyo wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ambayo imezinduliwa jana Upanga, jijini Dar es Slaam.
“Nawapongeza kwa huduma ambayo mnatoa kwa wateja wenu kikubwa nikuendela kuwa na mahusiano mazuri na wateja, kusikiliza maoni ya wateja pamoja na kushauriana na kubwa zaidi ni ushirikiano na wafanyakazi wenu,”amesema Kunenge.
Kampuni ya Puma imesajiliwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kampuni inayomilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia (Msajili wa Hazina, Wizara ya Fedha) pamoja na Puma Investment Limited kila moja ikiwa na umiliki wa hisa wa asilimia 50.
More Stories
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi