December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu wafariki ajalini Mwanza

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

WATU watatu wamefariki na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne katika Jiji la Mwanza.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Nyakato sokoni wilayani Ilemela baada ya roli lilolokuwa limebeba matofali kufeli break na kugonga magari matatu na kusababisha vifo hivyo.

Akizungumzia ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willboard Mtafungwa,alisema ajali hiyo imetokea leo Desemba 1,mwaka saa 2 kamili asubuhi.

Amesema miili ya watu wawili ilitambulika.

Mutafungwa ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kushindwa kufanya kazi kwa mfumo wa breki na kugonga magari hayo,yaliyokuwa yamesimama yakisubili taa kuwaka ili yaweze kuanza safari ya kutoka Nyakato kuelekea mjini Mwanza.

Amewataja watu waliofariki kuwa ni Shabani Ally (81) mmiliki wa gari namba T594 DNM,mkazi wa Nyakato,James Lukas aliyekuwa kwenye gari namba T604 CJK aina ya Toyota Hiace (22)mkazi wa Igoma na mwingine ambaye hajafahamika ni abiria wa roli namba T879.

Amesema majeruhi 18 walipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekouture na kituo cha afya Buzuruga ambapo 15 waliweza kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani na watatu bado wapo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando lakini hali zao zinaendelea vizuri.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kuwa wamebahatika kuwaokoa baadhi ya majeruhi waliokuwa wamebanwa na matofali yaliyokuwa kwenye roli.

“Tunawaomba madereva wawe makini katika eneo hili, maana kuna njia panda,mataa na kuna mtelemko mkali, wahakikishe gari wanazopewa hazina itilafu,ili kuepuka ajali,” amesema.