January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu mbaroni tuhuma za mauaji ya watu saba

Na. Ashura Jumapili, Timesmajira Bukoba,

Watuhumiwa watatu wa mauaji ya watu saba wa familia moja yaliyotokea Novemba 13 mwaka huu baada ya kula mbogamboga zenye sumu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera ambapo watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda ameeleza hayo Desemba 23,2023 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Bukoba ambapo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jenipher Petro Nyakindi (19),Mernes Petro (22) na Emmanuel Julius maarufu kama Noel (31) wakazi wa mtaa wa TRM kijiji ha Nyakanazi Kata Rusahunga Wilayani Biharamulo mkoani hapa.

Chatanda amesema kuwa vifo hivyo vilitokea kwa nyakati tofauti baada ya watu 11 wa familia moja kula chakula na mboga hizo Novemba 13 mwaka huu ambapo asubuhi ya Desemba 14 watoto watatu wa familia hiyo walianza kujisikia vibaya na kukimbizwa kituo cha afya Nyakanazi wakati wakiendelea kupatiwa matibabu walipoteza maisha.

Amesema baada ya watoto hao kupoteza maisha na wengine watatu waliokuwa wamebaki nyumbani walijisikia vibaya na kukimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Biharamo ambapo wawili walifariki Novemba 15 na baadaye pia vifo vya wanafamilia wengine wawili viliongezeka na kufanya idadi kufikia saba.

Pia amesema kuwa watuhumiwa hao baada ya kutenda kosa hilo walikimbia ambapo jeshi hilo kwa kushirikiana na raia wema waliendelea kuwatafuta ambapo walikamatwa wakiwa kwa kaka yao aitwaye Emmanuel Julius huko maeneo ya Bugengere kijiji cha Shinyanga “A” Kata Nyakukuru Wilaya Mbogwe Mkoani Geita.

“Wathumiwa walipohojiwa wamekiri kutenda unyama huo kwamba waliweka dawa za kienyeji zikiwa na sumu aina ya biazion inayotumika kuua wadudu ambapo waliiweka kwenye majani ya maharage maarufu kama musokolo baada ya kuituhumu familia ya Razaro Sanabanka kwamba wameiba kuku wao mmoja na kisha kumchinja,”ameeeleza Chatanda.

Hata hivyo jeshi hilo linawashukuru wananchi wote wa Mkoa huo kwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuwafichua waharifu hivyo akawaomba waendelee kutoa ushirikiano ili wanaojihusisha na vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.