January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Mbeya

WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili wakazi wa Kata ya Igurusi wilayani Mbarali na kujeruhi watu wengine watano kutokana na ugomvi wa kugombea ardhi kwa familia mbili.

Akizungumzia tukio hilo Januari 14,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema kuwa tukio hilo limetokea Januari 10,2025 majira ya saa 10.00 jioni ktongoji cha Shitanda Kata ya Luhanga wilayani humo.

Kamanda Kuzaga amewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Kuva Zengo(25)Lukeresha Mlawa (32) pamoja na Bulanda Mathias (25) wote wakazi w Kijiji cha Luhanga wilayani humo.

Aidha Kamanda Kuzaga amewataja waliouwawa kuwa ni Iddi Mjengwa(38) mkazi wa Igurusi,Maige Jifaru (44) mkazi wa Isunura na kusema kuwa katika vurugu hizo walijeruhiwa watu watano .

Ambapo amesema ugomvi huo ulitokea baina ya familia mbili ya Mzee Rafael Ramadhani Mjengwa mwenye hati namba MBL/420 iliyotolewa mwaka 1987 dhidi ya familia ya Mzee Malewa, uliosababishwa na mgogoro wa ardhi ambalo ni shamba lenye ukubwa wa ekari 1050.

Ambapo familia ya Mzee Malewa pia wanadai shamba hilo ni la familia yao kwani wamekuwa wakilitumia kwa kilimo na kulisha mifugo kwa muda mrefu.

Kuzaga amesema wakati familia ya Mzee Rafael Ramadhani wakiwa wanaendelea na maandalizi ya kilimo katika shamba hilo, ghafla walishambuliwa na kundi la watu wapatao 15 wanaodaiwa kuwa ni wa Mzee Malewa na kusababisha watu wawili kufariki na wengine watano kujeruhiwa.

Hata hivyo amesema,kutokana na tukio hilo, ufuatiliaji umefanyika ambapo Januari 13, 2025 majira ya saa 2.00 usiku katika kijiji na Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali,jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa kuhusiana na tukio hilo.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa jamii kuheshimu maamuzi ya mamlaka zilizopo ili kuepuka vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara kwa watu wengine.Na endapo upande mmoja haujaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa ni vyema kufuata taratibu za kisheria kwa kukata rufaa ili shauri lao liweze kusikilizwa upya.