November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania wayaishi maono ya Rais Samia kufanikisha kilimo chenye tija

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

TANZANIA kama zilivyo nchini nyingine Duniani imeendelea kushuhudia matukio makubwa ya hali mbaya ya hewa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mabadiliko haya yamesababisha ongezeko na ukubwa wa majanga yanayohusiana na hali ya hewa ikiwemo mafuriko, ukame, matukio ya upepo mkali na ongezeko la joto.

Pamoja na hali hiyo Tanzania inaendeleza juhudi mbalimbali katika kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na yale ya tabianchi.

Miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa upande wa kilimo ni kutaka wakulima kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.

Mwelekeo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wanahamia kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuhama kwenye kilimo cha kutegemea mvua.

Mfano mzuri ni kauli ya Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, aliyoitoa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Tanzania uliofanyika hivi karibuni nchini China, ambapo katika mkutano huo, Silinde alisema kuwa Rais Samia ametoa agizo kwa wakulima nchini kuanza kulima kwa kutegemea maji badala ya mvua.

Waziri Silinde ameeleza kuwa, kauli hiyo ya Rais Samia inahusu mkakati wa kukuza kilimo cha kisasa, ambapo wizara ya kilimo imepewa jukumu la kujenga mabwawa na kuvuna maji ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinafanikiwa.

“Hii ndiyo kauli mbiu yetu sasa, kama tulivyoelekezwa na Rais, kuhakikisha tunajenga mabwawa na kutumia maji kwa kilimo badala ya kutegemea mvua pekee,” alisema Silinde.

Akifafanua zaidi, Silinde alisema kuwa China imetenga kiasi cha dola bilioni 360 kwa Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Sehemu ya fedha hizo itaelekezwa moja kwa moja kwenye sekta ya umwagiliaji nchini Tanzania, ambapo mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima.

Aidha, Silinde alieleza kuwa katika kipindi hicho, Serikali itahakikisha kuwa miradi yote ya umwagiliaji iliyopo itakamilishwa na miradi mipya itaanzishwa ili kuwasaidia wakulima kote nchini. “Tumejipanga kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilishwa, na miradi mipya inaanzishwa ili kuwasaidia wakulima wetu kufikia malengo,” aliongeza.

Rais Samia anafanya hivyo kwa kutambua kwamba kilimo kinawagusa watu wengi wakiwemo wananchi wa hali ya chini kabisa, ndiyo maana amejikita kuboresha kilimo. Amekuwa akielekeza kutolewa kwa fedha kwa ajili ya kuongeza mtaji wa uanzisha benki ya ushirika.

Akizungumza na maofisa ugani na wanaushirika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma hivi karibuni alimwagiza Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande kwenda kulifanyia kazi ombi la kutoa asilimia 10 kwa ajili ya uanzishwaji wa benki ya ushirika, akiwapa sh. bilioni 5 ili kufikia asilimia 51 ya hisa katika benki hiyo.

“Bilioni 5 (shilingi) zipo njooni mchukue, na hii ni kwa sababu tunaharakisha benki iweze kuundwa kwa haraka iweze kufanya kazi ya vyama vya ushirika. Kwa changamoto yoyote njooni mtuone hatutaki benki hii ishindwe,” alisema. Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia Afrika ndilo bara linalotegemewa kuzalisha chakula, hivyo Tanzania haina sababu ya kutokuwepo katika nchi yenye uzalishaji wa chakula ili kulilisha bara hilo na maeneo mengine ya dunia.

“Hii ni fursa tuliyoipata Tanzania kutokana na matokeo yanayotokea duniani ya kutokuwa na usalama wa chakula. Tukifanya vizuri katika kilimo, vijana watajiajiri au kuajiriwa katika maeneo ya kilimo, ndiyo maana Serikali tumeelekea katika sekta hii ambayo ndani yake kuna kilimo mazao, ufugaji na uvuvi,” alisema.

Rais Samia anatambua wazi kwamba malengo yote ya Serikali ya kukuza kilimo pamoja na kuhamia kwenye kilimo cha umwagiliaji hayawezi kukamilika bila kuwa na maofisa ugani.

Anaweka bayana kwamba maofisa ugani wamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya kilimo. “Hawa ni mashujaa wasiosemwa na mtu, lakini uhakika wa chakula tunaojivunia, asilimia 128 ya utoshelezi wa chakula Tanzania unatokana na maofisa ugani, licha ya kusahaulika, lakini ndio watalaamu wanaotuletea uhai, usalama na uhakika wa chakula,” alisema Rais Samia.

Alisema matokeo ya ongezeko la tija, uzalishaji na mchango wa pato la Taifa unachangiwa na juhudi za maofisa ugani.

“Niliwashukuru wakulima kwa sauti kubwa, leo nawashukuru ninyi kwa sauti kubwa pia kwa mchango wenu muhimu,” alisema. Alisema maofisa ugani na ushirika wana jukumu kubwa la kuchochea uchumi wa Tanzania, ndiyo maana Serikali iliboresha mazingira yao ya kazi ikiwemo kuwawezesha vitendea kazi.

“Tunavyokwenda mbele nimeona matokeo chanya kwa maofisa ushirika na ugani kwenye sekta ya kilimo, hata lile la wakulima na wafugaji kukubaliana kukaa pamoja na kusema imetosha, mwanga umeonekana,” alisema.

Aliwataka maofisa ugani kutulia katika maeneo wanayopangiwa na Serikali ili kuwahudumia wananchi. Alisema lengo la Serikali kwa siku za usoni ni kuhakikisha kunakuwa na ushirika unaondeshwa kisasa, uwekezaji unafanywa kitalaamu ukilenga kumnufaisha mwana ushirika, siyo kumkandamiza.

Mwakilishi wa maofisa ugani, Enock Ndunguru amesema kumekuwa na kasi kubwa ya maendeleo katika sekta ya kilimo, ikiwemo maofisa ugani kupewa vitendea kazi.

Alimwomba Rais Samia kuzitengenisha sekta za kilimo na mifugo zilizounganishwa kuwa moja katika ngazi ya serikali za mitaa, akisema inaleta shida kwenye utekelezaji wa majukumu. Rais Samia amewataka mawaziri wa sekta husika kukaa pamoja kuangalia sheria, kuongeza au kubadilisha kwa lengo la kulifanyia kazi.

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe alisema awali maofisa ugani wa kilimo walisahaulika, lakini sasa hali imekuwa tofauti kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali.
Alisema wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021, bajeti ya ugani ilikuwa sh. milioni 682 lakini katika mwaka wa kwanza aliongeza hadi sh. bilioni 17.7

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, alisema maofisa ugani ni watu muhimu waliobeba matumaini ya kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kila mkulima wanayemsaidia au shamba wanaloelimisha ili kuwa na Tanzania yenye chakula cha kutosha na uchumi imara.

“Maofisa ugani ni madereva wa mabadiliko wakichochea mchakato wa uzalishaji bora, kufufua ardhi iliyokosa rutuba na kuleta matumaini mapya kwa mamilioni ya wakulima na wafugaji,” alisema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema maofisa ugani wa uvuvi na mifugo wamepata vitendea kazi zikiwemo pikipiki zaidi ya 1,500 zilizosambwa katika mikoa mbalimbali nchini. Pia mafunzo rejea ya teknolojia na maarifa ya kisasa yametolewa kwa maofisa ugani wa mifugo na uvuvi 3,600.

Mwishoooooooooooooooooooooooooooo