September 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania washauriwa kutopuuza dawa za asili

Na David John, TimesMajira Online, Njombe

WATANZANIA wameshauriwa kutopuuza matumizi ya dawa za asili, kwani dawa hizo zimekuwepo tangu enzi za babu zetu ambazo walikuwa wakizitumia na kuwasaidia kwa kiwango kikubwa kabla ya kuja dawa za kisasa.

Ushauri huo umetolewa mkoani Njombe leo kwenye maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambayo yanakwenda sambamba na maonyesho ya chakula na lishe, ambapo Mjalisiliamali na mtaalamu wa matabibu wa dawa za asili Rehema Said maalufu ‘Bisuya’ amesema, watu wanapuuza matumizi ya dawa hizo lakini kwa asilimia kubwa zinasaidia mno na huko nyuma ndio ilikuwa tiba halisi.

Amesema kupitia maadhinisho ya siku ya chakula duniani, wananchi wa mkoa wa Njombe wajitokeze kwa wingi kwenye viwanja vya Mji mwema vilivyopo mkoani humo ili kujipatia dawa tiba za magonjwa mbalimbali yanayowasumbua watanzania.

“Ndugu zangu waandishi habari huko nyuma babu zetu na mama zetu walikuwa wanazitumia sana dawa hizi na walikuwa hawapati magonjwa mara kwa mara kama ilivyo sasa na walikuwa na nguvu nyingi kuliko ilivyo leo, hivyo wananchi wanatakiwa kusema matatizo yao yanayowatatiza ili wapate dawa hapa,”amesema Bisuya.

Ameongeza, kupitia maadhinisho hayo wananchi watapata fursa ya kupata dawa za kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na changamoto ya macho, vidonda vya tumbo, tenzi dume, dawa za kuzibua mirija ya uzazi, Ngiri, chango kwa akina mama pamoja na dawa zingine watazipata kwenye maonyesho hayo.

“Nataka niwaeleze wanahabari wananchi bado wana maradhi mengi kwenye miili yao na maradhi mengine yanasabanishwa na aina ya vyakula ambavyo tunakula, kwani mafuta yanakuwa mengi, hali inayosababisha miili kupata shinikizo la damu, wakati mwingine kusumbuliwa na miguu kutokana na ulaji wa vyakula mbalimbali hivyo waje sehemu ambayo nilipo ili waweze kupata miti ya dawa, “amesema.