Na Mwandishi Wetu, timesmajira
MKURUGENZI wa Bodi ya Kahawa nchini Primius Kimaryo ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kunywa Kahawa kwani ina manufaa mengi.
Wito huo ameutoa jana katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania inauza nje asilimia 93 ya kahawa inayozalisha nchini na kiasi kikubwa kinaenda nchi za Japan na jamii ya Ulaya na nchi zingine kama Israel na Urusi.
“Sisi tunakunywa asilimia 5 mpaka 7 kwa wastani kwahiyo tunategemea uhamasishaji zaidi utaongeza Matumizi yetu mpaka asilimia 15 kama tulivyojiwekea. Tuna mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha migahawa inayotembea kwenye mitaa ya maonesho mbalimbali…hili ni eneo moja wapo ambalo tunawekeza hasa kwa vijana ili waendelee kufanya biashara ya kahawa.
“Sio hivyo tu serikali iliondoa gharama za leseni na tozo mbalimbali ili kutoa fursa ya wazalishaji wa kahawa kuweza kupata kipato kupitia zao hilo. Lakini pia tunatoa elimu za kiafya kwanini kahawa ni nzuri kwasababu kumekuwa na maneno mengi kwamba kahawa inaleta presha na matatizo mengine, kwahiyo tunaendelea kuelimisha,” amesema na kuongeza kuwa:
“Tukumbuke kuwa nchi kama Finland mtu mmoja anakula kilo 12 za kahawa kwa mwaka. Sisi huku mtu mmoja anakula si chini ya nusu kilo kwa mwaka kwahiyo kiwango hiki sio kikubwa kama kile,”.
Vilevile amesema kuwa serikali inakusudia kuzalisha tani 85,000 za kahawa kwa mwaka 2023/24 huku akibainisha kuwa Tanzania ina kahawa za aina mbili za robusta na arabika na kuzalisha kahawa 82,000 kwa mwaka 2022/23.
Amesema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye vioski vya unywaji wa kahawa kwenye vyuo mbalimbali nchini na migahawa, jambo ambalo litachangia kuongeza pato la Taifa na kukuza soko la ndani.
“Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye banda hilo wamesema kuwa, ikiwa wananchi wataelimishwa unywaji wa kahawa wanaweza kuongeza pato la Taifa na kukuza soko la ndani”alisema na kuongeza
“Serikali ilihamasisha ulimaji wa zao la kahawa jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa Kahawa,” amesema Inocent Mushumbusi mkulima wa kahawa kutoka Mkoa wa Kagera.
Amesema kuwa, wakulima wa zao Hilo wamekuwa wakipatiwa elimu ya uzalishaji wa zao hilo Ili waweze kuzalisha mazao bora ambayo yatakidhi viwango na kuingia kwenye soko la ndani na nje ya nchi na kuongeza mapato.
Naye Juma Abdalah Mkazi wa Chanika Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar Salaam, alisema kuwa, ikiwa serikali itatoa elimu Kwa wananchi kuhusiana na utumiaji wa Kahawa, soko la ndani litakua.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba