Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC)limesema litatumia kiasi cha dola za Marekani Milioni 200 sawa na jumla ya shilingi Bilioni 466 za Tanzania Kutekeleza Mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati na chini ujulikanao kama Samia Housing Scheme(SHS).
Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Meneja Habari na Uhusiano NHC,Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ya utekelezaji wa shughuli za Shirika hilo na Mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Saguya amesema kuwa mradi huo wa SHS unatarajiwa kutoa ajira 26,400 kwa watanzania ambapo ajira za moja kwa moja 17,600 na zisizo za moja kwa moja 8,800.
“Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na tunatamani watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo na asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar esSalaam, na asilimia 20 zitajengwa Dodoma huku mikoa mingine ikijengwa kwa asilimia 30,
“Nyumba hizi zitaanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam kutajengwa nyumba 500 na Medeli Jijini Dodoma nyumba100 na Mradi huu utakaotekelezwa kwa awamu nakutarajiwa kukamilika siyo zaidi ya mwaka 2025,”amesema Saguya.
Katika kutekeleza vipaumbele vingine Saguya ameeleza kuwa NHC itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Morocco square ambao ujenzi upo kwenye hatua ya uboreshaji wa mandhari (landscaping) na ufungaji wa lifti na viyoyozi kazi ambazo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu zitakamilika.
Aidha amesema sambamba na ujenzi huo, Shirika litaendelea na kukamilisha miradi ya Kawe 711 na Golden Premier Residence (GPR) iliyopo Kawe.
Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuanza utekelezaji wa Sera ya Ubia itakayoruhusu Sekta Binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya Shirika.
” Sera hii ina lengo la kuharakisha uendelezaji wa maeneo yaliyo wazi katikati ya miji yetu kwa kujenga nyumba za vitega uchumi na hivyo kuliongezea Shirika na nchi mapato makubwa.
Kuanzisha miradi mingine ya ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi;
Pia kuendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara nane Jijini Dodoma, wenye gharama ya Shilingi Bilioni 186 na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 na ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ujenzi wa majengo matano ya Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la TANZANITE Mirerani, ujenzi wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) na miradi mingine itakayojitokeza.
“Tutandelea kukusanya mapato na kodi ya pango ya nyumba za Shirika na tunatoa wito kwa wapangaji na wadaiwa sugu wa kodi ya pango ambao hadi kufikia Desemba 2021 wadaiwa sugu walifikisha shilingi Bilioni 26 hivyo tunawasihi kuhakikisha wanalipa kodi na malimbikizo wanayodaiwa kwa kuwa Shirika kuanzia sasa linajiandaa kukusanya kodi hii kwa asilimia 100.
Vilevile amesema NHC itaendelea kutekeleza Mpango Maalum wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za Shirika unaoishia mwaka 2027, kukarabati nyumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga, Mbeya, Mwanza, Singida na Kagera kwa gharama ya shilingi bilioni nane.
Pia kusaidiana na Wizara na wadau wa sekta ya Miliki nchini kubuni sera na sheria zitakazoifanya sekta ya miliki na nyumba kuchangia uchumi wa nchi yetu na Kazi hii wa meshaianza.
Saguya ameelez vipaumbele vingine kuwa ni kuendelea na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi wa nyumba za NHC hususan kokoto na matofali,kununua ardhi ekari 400 katika maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na akiba ya ardhi,kuendelea kuhamasisha wananchi na wapangaji wao kujitokeza Agosti 23, 2022 kuhesabiwa, Sensa ya watu na makazi ni kwa ajili ya kuleta maendeleo na kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya nyumba na Sekta ya Milki nchini. kupitia vyombo vya habari; vyombo vya habari ni mhimili muhimu wa upashanaji habari kwa Wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya Shirika.
Pamoja na hayo amezungumzia miradi yenye manufaa ya miradi ya ujenzi wa nyumba amesema kwa mradi wa SHS unatarajiwa kutengeneza mapato ya kodi mbalimbali za serikali mauzo ya nyumba TZS bilioni 50,ununuzi vifaa vya ujenzi bilioni 10,PAYE TZS bilion 17.8 , Kodi ya majengo TZS milioni 55, corporate Tax kutoka NHC na wajenzi wengine bilioni 77 na VAT bilioni 60.
Hata hivyo ameeleza kuwa Majukumu ya Shirika yanatekelezwa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Shirika wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25) ambao unalenga kusukuma mbele ujenzi wa nyumba zipatazo 10,000 na kuwezesha ukuaji wa sekta ya nyumba kupitia ushirikishwaji wa sekta binafsi.
“Shirika la Nyumba lina mtaji(capital base) wa Shilingi trilioni 5.04 hivi sasa unaotokana na rasilimali ya majengo yake 2,872 yenye nyumba(Units) zipatazo 18,654 zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini,”amesema.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu