Na Esther Macha, Timesmajira Online,Ileje
WAKULIMA wa kahawa Kata ya Luswisi wilayani Ileje mkoani Songwe wanaolima zao hilo maeneo yenye mteremko mkali wametakiwa kuzingatia matumizi bora ya udongo ,maji pamoja na taratibu zote ambazo zitazuia mmonyoko wa udongo utakao ondoa rutuba.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mtafiti Mwandamizi wa Afya ya udongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI)Dkt. Godstephen Maro wakati wa mafunzo ya Maofisa Ugani na Wakulima yaliyofanyika Kata ya Luswisi wilayani Ileje mkoani Songwe.
“Zipo njia nyingi za kuzuia mmonyoko mojawapo ni kuweka makinga maji ambayo yanazuia kasi ‘speed’ ya maji pamoja na udongo unaotiririshwa ili kufanya ule udongo uendelee kubaki katika eneo la shamba na rutuba yake kuendelea kubaki pia,”amesema Dkt.Maro.
Amesema kuwa ipo njia nyingine ya kuzuia mmonyoko huo kuwa ni matuta mkingamo ambayo ni muhimu kwenye maeneo ya mteremko mkubwa yote hiyo itategemea Ofisa Ugani mara baada ya kuona shamba la mkulima ndio sababu wamekuwa wakihimizwa kuwa karibu na wakulima wanapoanzisha mashamba mapya kwani wakitaka kuleta njia ya kuzuia mmonyoko wakati lilishanzishwa kunakuwa na ugumu.
Mtafiti huyo amewashauri Maofisa Ugani kuchukua nafasi zao kwa sababu ndio wenye dhamana ya kuwashawishi wakulima kufuata njia zinazofanywa kwenye kilimo.
“Kama Mkulima hafuati afuati njia hizo basi kuna mahali Ofisa Ugani alitetereka ile habari ya maofisa kuhangaika na upimaji wa nyama badala ya kwenda shambani kuangalia matatizo ya mashamba ya wakulima imepitwa na wakati inabidi ifike mahali sasa kubadilika kufanya kazi ya ukweli tuone tija ya ukweli shambani ili kuweza kuinua kipato cha mkulima,”amesema Dkt.Maro.
Meneja wa Kanda wa programu za utafiti kutoka TaCRI Dismas Pangalasi amesema wameleta watalaam wa kilimo wilayani Ileje katika Chama cha Msingi Chibila kupata mafunzo ya usimamizi na matumizi bora ya ardhi ili kuweza kuongeza ubora wa uzalishaji wa zao la kahawa katika Kanda.
“Tumeona tuwalete watalaam wote wa kilimo huku kijijini ili wakutane ana kwa ana na wakulima tunafahamu kwamba wanakutana na wakulima mara kwa mara lakini kuleta munganiko ili kuyaona matatizo katika uhalisia hususani matumizi ya aina bora ya kahawa ambayo inaustamilivu wa magonjwa wa aina ya kompakiti,”amesema.
Hata hivyo Pangalasi ameeleza kuwa kwa sasa gharama zimepungua sababu ya aina bora ya mbegu ya Kompakiti ambayo inastawi hata kwenye miinuko na maeneo ya tambalale.
Pia katika mafunzo hayo wamewajengea uwezo Maofisa Kilimo namna ya kutengeneza matuta mkingamo kwenye maeneo yenye miinuko mikali ili kuzuia mmonyoko wa udongo na uharibifu wa mazingira ili kutengeneza kilimo cha kahawa.
Akizungumzia kuhusu mwitikio wa wakulima amesema wengi wamehamasika kutokana na aina ya kahawa aina ya Kompakiti kwa sababu inazaa ndani ya muda mfupi katika eneo la Chibila na matarajio kwa watalaam ni kujifunza mbinu za kuzuia mmonyoko wa udongo kwenye kilimo kinacholimwa kwenye miinuko mikali.
Mratibu wa mradi wa kuendeleza zao la kahawa Nyanda za Juu Kusini (CODE_P)Rashid Mallya,amesema kuwa mradi huo ulianza mwaka 2020 ambao ni wa miaka minne unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na mashirika matano ambayo ni Agroforest,TaCri,Black Maendeleo,Ansaf pamoja na Caffe Afrika.
Amesema kuwa mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji na tija kwenye zao la kahawa na kupunguza utapiamlo kwa Nyanda za Juu Kusini na kuongeza lishe bora ambao umejikita zaidi kutumia mbinu za mnyororo wa thamani.
Mallya amesema kuwa wanafanya shughuli zao kwenye mradi kugusia kila hatua ya mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji shambani,uhifadhi, usindikaji ,uvunaji pamoja na masoko pia unahimiza matumizi ya kahawa ndani ya nchi.
Huku kitwakimu kahawa nyingi inayolimwa inaenda zaidi nje ya nchi walaji si Watanzania hivyo wanaendelea kuwahamasisha wazawa kwenye unywaji wa kahawa.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi