Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Kilimanjaro
SERIKALI imetaka wafanyabiashara mkoani hapa kuwa wazalendo na kuepuka ukwepaji wa Kodi hususan katika maeneo ya mipaka na nchi jirani.
Aidha vyombo vya ulinzi na usalama vimetakiwa kutumia mbinu za ziada ili kudhibiti wakwepaji kodi ikiwamo kuwakama wanaokwenda kinyume na maelekezo ya serikali.
Mkuu wa Wilaya wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Makori Kisare amesema hayo wakati anazindua wiki ya mlipa Kodi mkoani hapa ambapo pia ameipongeza hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kudai kodi bila kutumia nguvu.
Amesema wakwepaji wa kodi hurudisha nyuma jitihada za serikali katika kuendeleza sekta za afya,elimu,miundombinu,kilimo na masuala mengine ya ukuaji wa nchi.
Makori ametaka wananchi kudai risiti wakati wa kununua bidhaa huku wafanyabiashara wakihakikisha wanatoa risiti za kieletroniki (EFD) kwa wakati.
Awali Meneja wa TRA mkoani hapa, James Jilala amesema mamlaka imevuka malengo ya mapato kwa mwaka jana kutoka lengo la kukusanya bilioni 257.8 hadi bilioni 263.1 sawa na asilimia 102.
Amesema pamoja na malengo hayo mwaka huu wamelenga kukusanya bilioni 240.8 lakini hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka iliyoanzia Julai hadi Oktoba mwaka huu tayari wamekusanya bilioni 71.2 kati ya lengo la kukusanya bilioni 76 sawa na asilimia 52 ya lengo.
Meneja amesema bado TRA inakabiliwa na changamoto za mwitikio mdogo wa walipa Kodi, utoaji hafifu wa risiti za EFD pamoja na magendo hususani katika wilaya za Rombo na Moshi vijijini.
Ametaja maeneo yaliyokithiri kwa magendo kuwa ni Chekereni, Kahe wilaya ya Moshi pamoja na Moshi vijijini kwa ujumla wake ambapo wafanyabiashara wasio waaminifu hupitisha magendo.
“Katika njia hizi tunakamata zaidi mafuta ya kula,sukari,majani ya chai na vifungashio vya bidhaa mbalimbali,”amesema.
Naye Msemaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kilimanjaro, Ishaka Juma amesema wamehamasika kulipa kodi baada ya kupata elimu ya ulipaji kodi.
Amesema wataendelea kutoa taarifa za msingi ili serikali ikusanye kodi kwa mafanikio kwa maendeleo ya Taifa.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi