November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kuutunza mradi wa maji Butimba

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Wakazi wa jijini Mwanza wametakiwa kuutunza mradi wa chanzo cha maji Butimba huku wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),wakihimizwa kuwatumikia wananchi ili lengo la Rais Samia la kumtua ndoo mama kichwani lifanikiwe.

Wananchi takribani 450,000 wananufaika na mradi wa chanzo cha maji Butimba wenye uwezo wa kuzalisha lita za maji milioni 48 kwa siku hivyo kuongeza uzalishaji wa maji jijini hapa kutoka lita milioni 90 kwa siku na kufikia lita milioni 138 kwa siku.

Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda akimsikiliza Meneja Miradi wa MWAUWASA Mhandisi Celestine Mahubi wakati alipotembelea mradi wa chanzo cha maji Butimba

Utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 2021 na kukamilika Oktoba 2023,uliogharimu kiasi cha bilioni 71 uliotekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa usiamizi wa MWAUWASA.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo Agosti 12,2024 Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) Taifa,Mary Chatanda,ameeleza kuwa katika mradi huo amezunguka na amejionea mwenyewe,ameridhika mradi mzuri na fedha iliotolewa imeendana na thamani ya utekelezaji wa mradi huo.

“Adhima ya Rais Samia ya kumtua ndoo mama kichwani, tangu akiwa Makamu wa Rais ndio maana alivyoingia kwenye urais ikawa kazi rahisi ya kutafuta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendelea ya maji nchini,niwapongeze kwa mradi mzuri wa maji tuendelee kuutunza mradi wetu,”.

Meneja Miradi wa MWAUWASA Mhandisi Celestine Mahubi amesema mradi huo kwa sasa umetekelezwa kwa awamu ya kwanza na unazalisha lita za maji milioni 48 kwa siku.

Pia ameeleza kuwa MWAUWASA imejipanga kutekeleza upanuzi wa mradi huo kwa awamu ya pili ambapo itaongeza uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 144 kwa siku.

“Upanuzi huo utaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ikiwemo ujenzi wa matenki matano ya kuhifadhia na kusambazia maji maeneo ya Kisesa, Fumagila, Nyamazobe, Buhongwa na Usagara,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,ameeleza kuwa kwenye mradi wa chanzo cha maji Butimba uliopo Halmsahauri ya Jiji la Mwanza umegharimu takribani bilioni 71.

“Ninavyozungumza fedha zipo kwenye akaunti kiasi cha zaidi ya bilioni 41 kwa ajili ya kujenga matenki ya kusambaza maji kwa wananchi, kupitia mradi huu wa maji tumejenga tenki kubwa la maji Sahwa kwa kiasi cha bilioni 17,”.

 Pia ameeleza kuwa kuna fedha nyingi ambazo zimeletwa kwa ajili ya kupanua chanzo cha maji Capripoint chenye uwezo kwa sasa wa kuzalisha lita milioni 90 kwa siku,    ili kiongeze upatikanaji wa maji Wilaya ya Ilemela.