January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kutumia fursa ya Ziwa Victoria, kufanya kilimo cha umwagiliaji

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Mkoa wa Mwanza una eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji linalokadirwa kufikia hekta 36,000 huku kati ya eneo hilo ni takribani hekta 1635 tu, sawa na asilimia 4.5 ndizo zinatumika katika umwagiliaji.

Hivyo wito umetolewa Kwa wananchi wa Mwanza kutumia fursa hiyo ya uwepo wa eneo hilo na Ziwa Victoria kufanya kilimo cha umwagiliaji ili kukuza sekta hiyo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima,wakati akizindua maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima nane nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka wa 2022 inasema “Ajenda 10/30: Kilimo ni Biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

Malima ameeleza kuwa, kupitia kauli mbiu amewasihi wananchi na wakulima kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo kwa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Huku akiwahamasisha kutumia fursa katika sekta ya kilimo zinazopatikana ndani na nje ya Kanda ya Ziwa Magharibi mathalani zilizopo katika kanda hiyo ambazo zinaweza kuchangia katika ukuaji wa Sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na uwepo wa Ziwa Victoria ambalo linaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji.Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi hasa ukame na pia ufugaji wa samaki hasa kwa njia ya vizimba Kwani serikali inalenga kuona sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030.

“Fursa hii ikitumika vema inaweza kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo kwa kutumia uwepo wa Ziwa Victoria Kanda ya Ziwa Magharibi pia kutekeleza uchumi wa bluu, Mkoa wa Mwanza umedhamiria kutekeleza mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano (2021 -2026) kwa kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria ili kutumia sura ya eneo la maji lililopo katika mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera,”ameeleza Malima.

Hata hivyo ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegharamia mafunzo ya awali ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na kuainisha maeneo yanayofaa kwa ajili ya ufugaji.

Ambapo Halmashauri za Mkoa wa Mwanza zimeshaanza kutekeleza hadi sasa kuna vikundi 64 vya vijana vyenye jumla ya wanachama 640 vimesajiliwa na kujengewa uwezo katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa maandalizi ya maonesho hayo,Emil Kasagara ameeleza kuwa maonesho hayo ambayo yalianza rasmi kwa kanda hiyo mwaka 2017 yamekuwa yakikumbwa na chamgamoto mbalimbali hususan ukosefu wa miundombinu ya kudumu hali hiyo huongeza gharama za uratibu hasa wakati wa ujenzi au ukarabati wa miundombinu mara kwa mara.

Kasagara ameeleza hadi Agousti 3,2022 idadi ya washiriki walikuwa zaidi ya 228 ikijumuisha mamlaka za serikali za mitaa wenye shughuli kubwa na za kati, taasisi za fedha elimu,afya, kampuni za zana za kilimo,usambazaji pembejeo vinywaji na kampuni za mawasiliano.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima, akizungumza wakati akizindua maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima nane nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima nane nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)