January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kupiga kura na kuondoka vituoni

Ashura Jumapili TimesMajira online Kagera,

Wananchi wametakiwa kuondoka katika vituo vya kupigia kura pindi wanapomaliza kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo Novemba 27,2024.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa Novemba 27, mwaka huu katika kituo cha kupigia kura cha uwanja wa ndege mtaa wa Pwani Manispaa ya Bukoba baada ya kumaliza kupiga kura yake.

Amesema wananchi wazingatie taratibu na kanuni za uchaguzi wa serikali za mtaa wakipiga kura warudi majumbani wapumzike wasubiri matokeo asiwepo mtu yeyote wa kufanya vurugu sababu hiyo haiendani na taratibu na tamaduni na mila na desturi za watu wa Kagera kwani wanasifika duniani kote kwa ustaarabu, utulivu, busara na hekima.

“Mkoa wa Kagera hali ya ulinzi na usalama ni shwari pamoja na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha kuanzia asubuhi wananchi walijitokeza kwa wingi kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura”.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Siima amesema kwamba, wameweka utaratibu mzuri kwa makundi maalum kwa ajili ya kupiga kura kwani walikuwa hawasimami kwenye foleni wanapofika walikuwa wanaangalia majina yao na kuingia katika chumba cha kupigia kura.

Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Jacobo Nkwera, amesema vituo vya kupigia kura katika manispaa hiyo idadi yake viko 160 na manispaa inayo mitaa 66.

Ailine Ng’wanugu mkazi wa mtaa wa Pwani amesema utaratibu wa upigaji kura ni mzuri na katika kituo alichopigia kura watu walikuwa wanafika wanapiga kura na kurundi nyumbani.

Hata hivyo, Mkoa wa Kagera una wapiga kura zaidi ya milioni 1.5 na vituo vya kupiga kura vipatavyo 4,012, Bukoba mjini vipo vituo 160, Bukoba vijijini 526, Muleba vituo 801, Misenyi vituo 360, Kyerwa vituo 675, Karagwe vituo 631, Ngara vituo 436 na Biharamlo 423.