Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
MKUU wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala ametoa onyo kwa wafanyabiashara wilayani humo watakaouza sukari kwa bei tofauti na maelekezo ya serikali kwamba watakamatwa na kufikishwa mahakamani kisha kushitakiwa kwa uhujumu uchumi pamoja na kufutiwa leseni ya biashara.
Masala ameeleza kuwa kilo ya sukari wananchi waliokuwa wananunua kwa shilingi 1800,2000 imepanda mpaka shilingi 4000 hadi 5000, kutokana na mvua kuwa nyingi inayochangia viwanda vya ndani kupata changamoto katika uzalishaji kama vile ilivyozoeleka kwani miwa imekuwa na maji mengi hivyo kushindwa kutoa bidhaa hiyo.
Ametoa onyo hilo Februari 28, 2024,wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu katika kikao chake cha kwanza cha ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Wilaya hiyo kilichofanyika kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo.
Ameeleza kuwa serikali haijakaa kimya ili kumlinda mlaji na mwananchi kupitia Wizara ya Kilimo, Waziri ameomba kibali cha kufungulia na kutoa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kama dharura ili kuziba mwanya wa viwanda vya ndani.
Hivyo baada ya zoezi hilo wapo wasambazaji wakubwa waliopewa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi wakiwa wamepunguziwa kodi na kuondolewa masharti ili wao waje wauze kwa wasambazaji wa rejareja ambao wanawauzia wananchi wa kawaida lakini wapo wanaendelea kuficha sukari ndani ili waendelee kuuza kwa bei ya juu hivyo watakao enda ndivyo sivyo sheria ipo wazi.
“Kwa kuliona hilo serikali imetoa bei elekezi ambayo imetofautiana kimkoa,Mkoa wa Mwanza kilo ya sukari inapaswa kuwa 2650 mpaka 3000, kwa bei ya jumla na kwa rejareja ni shilingi 2800 hadi 3200,”.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Buswelu Lidia Hugo, ameeleza kuwa hali siyo nzuri kwani kipato kipo pale pale lakini sukari imepanda bei jambo ambalo linawapa wakati mgumu.
“Naomba serikali ifuatilie bei hiyo elekezi ambayo wameelekeza kwa wafanyabiashara ili wananchi tusiumue maana ilitoka maagizo na kuto fuatilia itakuwa haijatusaidia sisi wananchi,”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi