Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
WATU watakaolala nyumba za wageni (Gesti) siku ya Sensa ya Watu na Makazi watafuatwa huko huko na makarani wa sensa kwa ajili ya kuhesabiwa.
Hayo yamesemwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya Sensa ya Watu na Makazi.
“Watu wote watakaokuwa wamelala gesti, hotelini watafuatwa na makarani wa sensa kwa ajili kuhesabiwa ikwemo na wale wote watakao safiri maeneo mbalimbali,” alisema Dkt. Chuwa.
Alisema siku hiyo usiku majira ya saa 6 na dakika moja makarani wa sensa wataanza kuhesabu kwenye gesti, hotelini, stendi na maeneo mengine yanayohusisha safari.
Aidha, Dkt. Chuwa alisema wageni wote kutoka mataifa mbalimbali ambao siku hiyo ya sensa watakuwa wamelala nchini watahesabiwa na kuchambuliwa baada ya sensa kujua idadi yao na idadi kamili ya wazawa.
Alisema kuwa,licha ya sensa hiyo kuhesabu watu wakiwemo wenye ulemavu, watoto wa mitaani, lakini pia itagusa sekta nyingi kama vile makazi ya watu zikiwemo nyumba na aina mbalimbali za mifugo.
Mkutano huo wa wadau ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya Mkoa huo, Anthony Mtaka ulihudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Wakati huo huo, karani yeyote wa Sensa atakayetoa siri ya mtu wakati wa Sensa ya Watu na Makazi atashtakiwa na kuhukumiwa kulipa sh. mil. 10 au kufungwa miaka miwili ama vyote kwa pamoja.
Adhabu hiyo imeelezwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Chuwa wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi.
“Uzuri sheria iko wazi kwa kosa hilo, hivyo si vizuri kwa karani wa sensa ambaye amepewa mafunzo yakiwemo ya maadili ya kutunza siri za anaowahoji halafu akafanya vinginevyo,” alisema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu mmoja wa wadau wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo ambaye alielezea hofu waliyonayo kwa baadhi ya makarani wa sensa kutoa siri walizohojiwa jambo ambalo alidai linasababisha wengi wao kusita kueleza ukweli.
Sensa ya Watu na Makazi inatarajiwa kufanyika Agosti 2022 ambapo uzinduzi utafanywa na Ris wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Makao Makuu ya nchi Dodoma.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha