December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakaofanya udanganyifu matumizi ya EFD kuchukuliwa hatua

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

SERIKALI imesema haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara nchini, watakaobainika kujihusisha na udanganyifu wa matumizi yasiyo sahihi ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) pamoja na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wasiyo waaminifu katika ukusanyaji wa mapato.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande, alipokuwa akiitimisha wiki ya EFD iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Katika wiki hiyo, iliwahusisha wafanyabiashara kutoka wilaya hiyo, lengo likiwa ni kuwataka waendelee kutumia mashine za EFD kwa usahihi pindi wanapouza bidhaa zao kwa kutoa risiti ya Kielektroniki kwa wateja.

Chande, amesema kuwa, kuna baadhi ya maofisa wa TRA wameonekana kutokuwa waaminifu, ambapo imedaiwa kuwa wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wachache wasiyokuwa waaminifu kuziharibu mashine huku wakijua kuwa kufanya hivyo kunaikosesha Serikali mapato kama inavyotakiwa.

“Wajue serikali ina mkono mrefu kwaio kama tukiwabaini tutawachukuliwa hatua kali dhidi yao, kwani kufanya hivyo ni sawa sawa na wale wahujumu uchumi, kupitia wiki hii natumai tumejifunza mengi juu ya matumizi ya EFD, ninaomba tukayafanyie kazi na kuendelea kutoa elimu kwa wengine wasiyo na uelewa,” amesema Chande.

Pia, Chande amewataka maofisa hao kukusanya mapato halali pindi wanapowatembelea wafanyabiashara ili Serikali iweze kunufaika kutokana na mapato hayo.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya EFD Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kupitia uhusiano mzuri na ushirikiano uliopo baina ya TRA,wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo,machinga na ofisi yake kwa pamoja wameweza kuleta mafanikio ya kuongeza ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo tofauti awali.

“Nawashukuru sana kwa kufanikisha hili,hivyo naomba kupitia wiki hii tunayoiadhimisha leo, wote kwa umoja wetu twende tukahimize na kuwa na matumizi sahihi ya EFD,”amesema Mpogolo.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata, amewataka watanzania kuwa na utaratibu wa kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa, ili Serikali ipate mapato mengi yatakayo saidia kuongeza nguvu katika miradi mikakati ikiwemo uboreshwaji wa vituo vya afya, upatikanaji maji safi na salama, elimu na miundombinu ya barabara za ndani na barabara kuu.

“Ni vyema wananchi wakawa na mazoea ya kudai risiti pindi wanapoenda kudani kununua kitu..dai risiti kwa maendeleo ya taifa, kwani kwa kufanya hivyo Serikali itajipatia mapato ambayo yataenda kusaidia katika miradi mbalimbali ikiwa pamoja na uboreshwaji wa vituo vya afya, upatikanaji wa maji safi na salama, elimu na miundombinu ya barabara za ndani na barabara kuu,”amesema Kidata.

Baadhi ya wadau waliohudhuria katika maadhimisho hayo, wanaojihusisha na uuzaji wa mashine za EFD, Timoth John, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na teknolojia mahususi ya upatikanaji wa risiti kwa njia ya simu, amesema huduma hiyo itamuezesha mfanyabiashara kumiliki huduma hiyo ili aweze kuuza bidhaa zake bila matatizo yoyote.

Pia ameongeza kuwa, huduma hiyo itamsaidia mfanyikabiashara huyo kuendelea kuuuza bidhaa zake hata bila ya kuwa na mashine ya EFD.Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Kodi yetu kwa maendeleo yatu, na EFD risiti yako kwa ulinzi wako”.