November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watafiti wa chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) wahofia kutoweka kwa wadudu wachavushaji 

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

IMEELEZWA kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa chakula pamoja na wadudu wachavushaji ambao ni muhimu kutokana na kuchangia katika uzalishaji wa mazao pamoja na kuboresha afya ya mazingira.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa chuo cha MUST, Dkt. Fredrick Ojija wakati wa uwasilishwaji wa tafiti anazofanya katika chuo hicho kwa wananchi na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Stela farm iliyopo katika eneo la Iwambi Jijini hapa .

Dkt. Ojija amesema  kuwa wadudu wachavushaji ni muhimu lakini wananchi walio wengi hawafahamu na hivyo kushindwa kuwahifadhi kutokana na kutojua umuhimu wake.

“Katika chuo chetu cha MUST tumekuwa tukifanya tafiti mbali mbali lengo likiwa ni kusaidia na kutoa elimu kwa jamii. Hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kupungua kwa chakula pamoja na kupungua kwa wadudu wachavushaji ambao ni muhimu kwasababu huchangia katika uzalishaji mazao ya chakula.

Aidha amebainisha kuwa  Chuo  cha MUST kimekuwa kikitoa fedha kwa watafiti wake ili wafanye tafiti kwa lengo la kusaidia jamii na kutoa elimu kwa wanafunzi, pia kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya wadudu wachavushaji ili wasiweze kupotea mashambani na katika mazingira tunayoishi “amesema  Dkt. Ojija’’.

Aidha Mhadhili huyo amesema  kuwa kwasababu wananchi hawajui namna ya kuwahifadhi wadudu hao inabidi wafike kwa wananchi kutoa elimu kupitia mradi huo juu ya umuhimu wa kutunza mazingira. 

Ameongeza kuwa endapo wadudu hao wakishindwa kutunzwa na kupotea kuna hatari ya kuongezeka kwa baa la njaa kwani uzalishaji wa mazao yanayotegemea uchavushaji utapungua.

Akielezea zaidi Dkt. Ojija amesema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa wadudu wachavushaji wanaendelea kupungua duniani na wadudu hao wanachavusha mimea zaidi ya laki tatu duniani, na asilimilia 90 ya mazao ya chakula hutegemea wadudu hawa.

Amesema  kama hatutatunza mazingira na wadudu hawa kupungua kwa kiwango kikubwa mwisho wa siku wananchi watatumia gharama kubwa ili wazalishe mazao kwa wingi .

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Sayansi Asilia, Dkt. Eliezer Mwakalapa amesema kuwa wanakishukuru chuo hicho kwa kujali watafiti na kuwawezesha kifedha ili kufanya utafiti na kutoa elimu kwa wananchi juu ya wadudu wachavushaji.

Aidha Dkt. Mwakalapa alisema viwatilifu vimekuwa vikichangia upotevu wa wadudu wachavushaji kutokana na matumizi mabaya ya viwatilifu ambapo unatumika bila uangalifu na hivyo kusababisha upotevu wa wachavushaji na upungufu wa mazao.

Ignas Mgalla ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Stela farm iliyopo Iwambi Jijini Mbeya amesema anashukuru watafiti wa chuo cha MUST kwa kuwapatia elimu juu ya wadudu wachavushaji kupitia elimu hiyo kwa maana wadudu hao wana faida kubwa kwa maisha ya binadamu.

Mwanafunzi mwingine wa kidato cha nne, Catherine Shilanda ameshukuru kwa kupata elimu nzuri kutoka kwa watafiti wa chuo hicho kwani awali walikuwa wanaona wadudu kama nyuki kama adui hivyo kuamua kuchukua jukumu la kuwateketeza kwa kuona hawana manufaa.

“Mdudu nyuki tulikuwa tunamuona kama adui kwasababu ya kutuuma, hivyo basi natoa wito kwa jamii kuwa wadudu hawa wachavushaji wana faida nyinyi ikiwemo kuongezeka kwa mazao pamoja na kupendezesha mazingira, tuwatunze  na kuwathamini kwani elimu tuliyopewa na watafiti kutoka chuo cha MUST ina umuhimu mkubwa  katika mazingira kwani wametukomboa kifikra kwa ujumla tumefurahi tumepata elimu nzuri juu ya wadudu wachavushaji”alisema.

Dkt. Ojija alishukuru menejiment ya chuo cha MUST kwa kufadhiri utafiti wake juu ya wadudu wachavushaji na kuomba wadau wengine wajitokeze kusaidia kwa namna yoyote kuendeleza utafiti huu.  

Dkt.fredrick Ojija akiwaonyesha wanafunzi juu ya wadudu wachavushaji kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Stela Farm
Dkt .Ojija akitoa somo kwa wanafunzi
Dkt.Eliezer Mwakalapa akitoa elimu namna ya kuwahifadhi wadudu hao
Wadudu ambao wanahofiwa kutoweka