November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu waonya watoto kuamshwa mapema kupelekea kuchukia masomo

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

MFUMO wa baadhi ya Shule za msingi na zile za awali hususani zinazomilikiwa na taasisi na watu binafsi, kuwawahisha watoto Shule majira ya saa 11.00 alfajiri, hujenga usugu kwa watoto na wengine kuichukia Shule.

Aidha baadhi ya wanafunzi hao wakiwamo wenye umri wa Chini ya miaka nane huona suala la elimu ni adhabu kwani Muda huo walistahili kuwa bado wamelala.

Hayo yamesemwa na baadhi ya wakazi wa kata ya Kaloleni Manispaa ya Moshi, Rashid Mchata na Swalehe Waziri wakizungumzia mpango jumuishi wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto MMMAM.

Mchata alisema mtoto wake ameanza kuichukia Shule haswa pale anapopewa adhabu mara anapokosea darasani lakini chanzo ni pale anapowahishwa Shule licha ya masomo kuanza saa 1:30 au 2:00 asb.

Wazazi na walezi waliomba Mamlaka husika kutoa muongozo Mzuri ili kuepuka kujenga kizazi kitakachoichukia elimu kutokana na sababu zinazozuilika.

Akizungumzia hoja hiyo, afisa ustawi wa jamii kiongozi katika Manispaa ya Moshi, Dancan Mgati alikiri kuwapo kwa mfumo huo lakini akaongeza kuwa wamekuwa wakitoa elimu kuhusu malezi sahihi ya watoto.

“Hakuna Sheria inayoelekeza muda wa kufika shule bali miongozo inataja siku za masomo, kufunga na kufungua Shule…hili la kuingia Shule ni makubaliano ya wazazi na shule husika” alisema.

Hata hivyo Mgati alikiri kuwa suala la watoto kuwahi Shule majira ya alfajiri huchangia baadhi yao kuichukia Shule na hivyo kuathiriri viwango vyao vya taaluma.

Naye mmoja wa wamiliki wa Shule ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema mfumo wa kuwahi Shule umewekwa kulingana na jiografia ya makazi ya wanafunzi.

“Hili la kuchukua watoto saa 11 alfajiri tumelenga wawahi darasani ifikapo saa 1:20 au 2:00 masomo yaanze….utakumbuka Shule ndiyo yenye jukumu la kuwachukua nyumbani ikilinganishwa na wale wanaokuja wenyewe kila siku” alisema.

Kuhusu suala la baadhi kuichukia Shule alisema jambo Hilo ni nadra kwani wanao walimu na walezi wanaifahamu namna sahihi ya kuwwhudumia watoto wadogo.