June 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu Manispaa Tabora wapongezwa

Na Allan Kitwe, Tabora

WATAALAMU wa Halmashauri ya Manispaa Tabora wamepongezwa kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo na kuandaa vizuri na kwa usahihi taarifa za matumizi ya fedha zote zilizopokelewa na za mapato ya ndani.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha kwenye kikao cha mwisho cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo.

Amesema kuwa usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo umepelekea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuipa halmashauri hiyo hati safi (unqualified opinion).

‘Nawapongeza sana Mstahiki Meya, Naibu Meya, Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji na Wataalamu wote wa halmashauri ya manispaa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na usimamizi thabiti wa fedha za maendeleo’, amesema.

Mtondoo amefafanua kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ndani ya manispaa hiyo yamechochewa kwa kiasi kikubwa na ufanisi wa wataalamu wake, ushirikiano na kufanya kazi kwa kujituma.

Ametoa wito kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa huo na Wataalamu wote kuendelea kufanya kazi kama timu moja na kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo katika idara au kitengo chake.

Awali akiwasilisha taarifa ya CAG katika kikao hicho kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkaguzi wa Nje kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hamza Zonga amepongeza halmashauri hiyo kwa kufanyia kazi hoja zote.

Ameeleza kuwa ripoti kuu ya CAG ilikuwa na jumla ya hoja 41 zilizokuwa zinahitaji ufuatiliaji ambapo hoja 23 sawa na asilimia 56 zimefanyiwa kazi na hoja 18 sawa na asilimia 44 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kutoa hati safi au inayoridhisha haimaanishi kwamba halmashauri husika ina mfumo wa udhibiti wa ndani wenye ufanisi wa asilimia 100 bali inamaanisha hakuna jambo lolote kubwa lililobainika la kumfanya CAG atoe hati yenye shaka.

Mstahiki Meya wa manispaa hiyo anayemaliza muda wake Ramadhan Kapela amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za kutosha ili kutekelezwa miradi ya wananchi na wataalamu kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo.