April 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasira:Ilala kuna watu wameanza kampeni

*Asisitiza kuwa wanajulikana ikiwemo watumishi

*Asema uchaguzi utafuata taratibu na vigezo kwa wagombea

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Steven Wasira,amesema kuna watu wameanza kampeni huku wengine ni watumishi,ambao wamekuwa wakipita kudanganya wananchi huku wakiwapa fedha.

Wasira,amesema hayo wilayani Ilala katika mkutano mkuu maalum wa Jimbo la Ilala ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mussa Zungu,ambapo amesema watu hao wanajulikana.

“Nawaomba Wabunge wengine mkajifunze kwa Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa zungu ana uhusiano mzuri na wananchi,ila kuna watu wameanza kampeni mapema wengine watumishi wanapita wanatoa shilingi 100,000 kwa wapiga kura wanajulikana.Uchaguzi wa mwaka huu unafuata taratibu na vigezo kwa wagombea,”amesema Wasira.

Amesema,chama hicho kinaendelea kudumu sababu kizazi kimoja kinarithi kingine na sasa CCM imepanua demokrasia wapiga kura wameongezeka huku akiwataka watakaogombea nafasi za Ubunge na Udiwani wasitoe rushwa kwani chama hicho kinazuia kufanya hivyo.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CCM tayari imeisha mteua mgombea nafasi ya Urais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mgombea mweza nafasi ya Makamu wa Rais Dkt.Emanuel Nchimbi,ambao watachuana na vyama vingine vya siasa,hivyo amewataka wanaCCM kujianda kwa ushindi wa kishindo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema baadhi ya mambo aliyotekeleza katika uongozi wake ujenzi wa zahanati ya kisasa Bungoni Mtaa wa Mafuriko ,Kituo cha afya Mchikichini.

Pia katika sekta ya elimu,barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami ikiwemo ya Moshi,Nyati ,Chunya na Mwanza huku wananchi wa Jimbo hilo wakipata maji safi na salama kwa asilimia 100.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar- es-Salaam Omary Kumbilamoto,amesema,miradi 19 ambayo ilikuwa imekwama sasa inaelekea kukamilika.