February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasira: CCM itashinda dola kwa kura si kwa bunduki

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Busega

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu Chama kitaendelea kushika dola kwa wingi wa kura na si mtutu wa bunduki.

Pia, amesema kuwa CCM imebeba maono na fikra za ukombozi wa watu na kwamba itaendelea kuwa wakili wa kuwatetea Watanzania huku akibainisha kuwa maendeleo huja na changamoto.

Wasira aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu alipokuwa akielekea jijini Mwanza.

“Katika uchaguzi mkuu mwaka huu CCM tutashinda maana hakuna wa kupambana na CCM. Mtaji wetu ni kushika dola na dola hatuishiki kwa bunduki bali tunaishika kwa kura na kura zinapigwa na wana CCM na wasio wana CCM,” alisema.

Akieleza zaidi kuhusu uimara wa CCM, Wasira alisema Chama hicho ni muungano wa vyama vilivyoleta ukombozi katika nchi uliotokwna na vyama vya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP).

“Kwa hiyo wanachama na viongozi wa Chama tunabeba maono ya vyama vilivyopita na sisi ndio tunaendeleza kazi ya uhuru, kuleta mabadiliko katika maisha ya watu.

“Wako watu wengine wako Ulaya wengine wako hapa ‘maajenti’ wao, wanasema CCM imekaa sana nami nawauliza tulivyodai uhuru tulisema tutakaa mpaka lini?

“Tulidai uhuru kwa sababu kuna ajenda ya kubadili maisha ya watu, na kubadili maisha ya watu hakuna mwisho kwa sababu maendeleo yanazaa matatizo mapya.

“Tunaendelea kujenga Tanzania yenye maendeleo kuondoa matatizo.Nataka kuwaambia Chama chetu ni kwa ajili ya kuwakomboa watu ambao hawana uwezo na hata wakipata matatizo hawawezi kuweka wakili, hivyo CCM ndio wakili wao.

“Tunataka Chama hiki kiwe wakili wa watu wote, tuwe tumaini la makundi yote, tunataka liwe tumaini la vijana wa Tanzania, tunataka liwe tumaini la wafanyabiashara, tumaini kwa mama lishe, wamachinga.

Kwa mujibu wa Wasira, CCM ni chama cha wanachi na kuanzia sasa muda mwingi utatumika kuzungumza mambo ya watu.

“Tunataka kutumia muda zaidi kuzungumza mambo yanayohusu watu.Tunataka kujua watu wana matatizo gani na vikao vyetu vizungumze matatizo ya watu na kutatua kero,”alisema Wasira

Akifafanua zaidi alisema hata muundo wa mfumo uliopo unataka Chama Cha Mapinduzi kiwe daraja kati ya watu na Serikali ili Chama kijue matatizo ya watu na kimalize yanayowezekana na yanayohitaji dola aagizwe mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya kuhakikisha ufumbuzi wake.

“CCM ni wakala wa watu hivyo tuhakikishe dhuluma hailelewi katika maeneo yetu, Chama chetu kilipoanza miaka 48 mimi nilikuwa mjumbe katika mkutano ulioanzisha CCM.

“Tulikubaliana kuunda chama chenye nguvu kimuundo na fikra ili kiwakombe watu wanaohitaji ukombozi watu ambao hawawezi kuajiri wakili Chama hiki kiwe wakili wao na hiyo ndio kazi tunayoifanya katika ngazi ya shina hadi halmashauri kuu ya Taifa,”aliongeza.

Hivyo Wasira alisisitiza wana CCM wazungumze mambo yanayohusu maslahi ya watu na wao mtaji wao watu na ukiwanyang’anya watu umekuwa umewanyang’anya mtaji

Kuhusu wagombea ndani ya Chama hicho alisema tayari wameshapata wagombea wao hivyo wanawasubiria watani zao(wapinzani)na kwa hali ilivyo katika vyama vyao Ikulu wataiona kwenye luninga.

“Mpaka hivi ninaposimama hapa hakijapatikana chama mbadala wa kupambana na CCM hata CHADEMA imebakia nusu halafu watushinde. CCM ushindi ni lazima na ushindi unaotokana na kura.”