February 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasira ‘aipiga nyundo ‘No reform no election

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Mwanza

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinajisumbua na msemo wake wa “No reform no election’ ((kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi)) kwani uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa.

Amesisitiza kuwa hakuna chombo chochote cha Serikali wala chama cha siasa kinachoweza kuahirisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hivyo Watanzania wajiandae kwa uchaguzi huo.

Wasira amesema watu wanaotoa hoja kwamba uchaguzi mkuu hautafanyika hadi yafanyike mabadiliko ya Katiba wanajisumbua kwa kuwa makubaliano yalishafanyika madiliko ya Katiba yatafanyika baada ya uchaguzi, hivyo hakuna anayeweza kuahisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa namna yoyote.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, jana, Wasira alisema kuwa kuhusu suala la Katiba mpya makubaliano yalifanyika na kukubalika kuwa hilo litafanyika baada ya uchaguzi mkuu.

“Tumekubaliana tumalize uchaguzi, zile sheria za uchaguzi zifanyiwe marekebisho, wabunge wanajua sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani imepitishwa na Bunge, sheria ya vyama vya siasa imefanyiwa marekebisho na imepitishwa na Bunge.

“CHADEMA wamekuwa na msemo wao maarufu ‘no reform no election’ (kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi), sasa mimi hapa nasema uchaguzi mkuu lazima utafanyika.

Wanaosema uchaguzi hautafanyika mpaka mabadiliko yafanyike wanajisumbua, uchaguzi utafanya na Watanzania wajiandae.

“Sisi ni Chama cha siasa lazima tufanye uchaguzi ili tuendelee kuleta maendeleo ya Watanzania. Halafu wamekuwa wakisingizia CCM tunaiba kura wakati hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 wameshindwa kuweka wagombea. Tunawaambia hatuna tunachoogopa,” alisema Wasira

Alisisitiza kuwa sio chombo cha serikali wala chama cha siasa ambacho kina uwezo wa kuhairisha uchaguzi na kufafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kisheria inalo jukumu la kutangaza tarehe ya uchaguzi, lakini haina uwezo wa kuhairisha.

“Na kama kutakuwa sababu ya uchaguzi mkuu kusogezwa mbele au kuahirishwa basi ni kwa sababu ya uwepo wa vita lakini kwa bahati nzuri nchi yetu haina vita, iko salama na kazi ya kuleta maendeleo inaendelea.

Hivyo hakuna chama cha siasa kinaweza kuahirisha uchaguzi na kuhusu suala la mabadiliko ni la kisheria.

“Unataka mabadiliko utafanya peke yako? hivyo niwahakikishie Watanzania uchaguzi upo na wajiandae kwa uchaguzi mkuu na wana CCM wajiandae kwa kushinda kwa kishindo na kushika dola,” alisema.

Kuhusu utekelezaji wa Ilani, Wasira alisema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan utekelezaji huo umefanyika kwa kiwango kikubwa na wananchi ni mashahidi kwa yale ambayo yamefanyika katika maeneo yao.

“Moja ya ajenda ya mkutano mkuu uliofanyika Dodoma Januari 18 hadi 19, mwaka huu, ulikuwa na ajenda tatu na moja ya ajenda ilikuwa kusomwa kwa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mkuu ya mwaka 2020 hadi 2024. Kazi kubwa imefanyika katika kuleta maendeleo nchini.

“Miradi iliyotekelezwa imeonekana, kulikuwa na mgao wa umeme lakini kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere hivi saa mgao umekwisha. Hapa Mwanza kulikuwa na changamoto ya mgao na sasa tunaambiwa mambo yamekuwa sawa. Kazi inaendelea.

“Rais Samia alilirithi kazi ya kujenga reli ya SGR na wapo waliokuwa wanasema kazi hii haiwezi kuendelea.

Wakati Rais Dkt. John Magufuli anafariki ujenzi wa reli hiyo ulikuwa hatua za awali lakini tayari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ujenzi umekamilika na sasa reli hadi Makutopora imekamilika na ujenzi unaendelea na baada ya miaka miwili reli hiyo itakuwa imefika Mwanza.

“Dkt. Samia tunampa mitano kwa sababu ile reli baada ya miaka miwili itatoka Dar es Salam mpaka Mwanza itakuwa tayari na ujenzi utaelekea hadi Kigoma.

Pia reli ya SGR itakwenda Tabora,” alisema.
Aliongeza kuwa, mradi mwingine mkubwa ambao Rais Samia ameurithi ni kujenga daraja la Busisi ambalo limepewa jina la Magufuli na ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 99 na baada ya miezi michache litaanza kufanya kazi.

Kuhusu huduma za jamii kuna kazi kubwa imefanyika ikiwemo ya kujenga miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.