December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasiolipa kodi ya pango la ardhi kuchukuliwa hatua za kisheria

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema itawachukulia hatua za kisheria ikiwemo kufuta umiliki,kupiga mnada na kumilikisha viwanja vilivyopimwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji kutoka kwa  wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo  Afisa Ardhi Mkuu kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Biswalo Makwasa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu umiliki ardhi kwa viwanja vilivyopimwa pamoja na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi amesema Wizara hiyo imetoa siku 60 kwa wale ambao hawajalipa  kodi ya pango la ardhi na waliopimiwa viwanja na hawajamilikishwa  kuwasilisha maombi ya kumilikishwa viwanja na wasipofanya hivyo   Serikali itachukua hatua hizo za kisheria.

“Wizara inatoa muda wa siku 60 kuanzia tarehe 5 mwezi wa pili mwaka huu kwa wale wote wale walipopimiwa viwanja wanawasilisha maombi  ya kumilikishwa  na wenye milki za ardhi wahakikishe wamelipa kodi ya pango la ardhi,”amesema.

Amesema wamiliki wa ardhi wanakumbushwa wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi ya pango la ardhi.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Denis Mesamu amesema kutokana na wamiliki wa ardhi kusuasua Wizara kama ilivyo na utaratibu wake iliwapelekea hati za madai wa miliki wasiolipa kodi ili kuhakikisha wanalipa kwa wakati.

Amesema utaratibu huo umeonesha matunda huku akitolea mfano kwa Mkoa wa Dodoma ambapo  ulipaji wa kodi ya ardhi umeongezeka katika kipindi cha Disemba mwaka jana wiki mbili za kwanza ulipaji wa kodi ulikikuwa wamiliki 200 lakini baada ya kuanza zoezi la kupeleka hati za madai walifika mpaka 800 kwa wiki na mapato yalitoka shilingi milioni 40 kwa wiki mpaka milioni 102.

Kutokana na hayo ametoa rai kwa watanzania wote wanaomiliki  kulipa kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kieletroniki kwa kutumia simu  kwani ni rahisi na ni rafiki pia kufanya hivyo ni kuiingizia Serikali mapato kwajili ya maendeleo ya nchi.

“Bado kumekuwa na changamoto kwa watanzania kushindwa  kutofautisha kati ya  kodi ya pango la ardhi na kodi ya majengo  ambapo watu hawafahamu kuwa  kodi ya majengo  inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwa sasa  inakusanywa  kupitia mita za luku za umeme,”amesema.

Ameeleza kuwa kodi ya pango la ardhi inakusanywa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mifumo ya Kieletroniki hivyo amewaomba wananchi wote wanaomiliki ardhi ambaye anadaiwa  kulipa kodi hiyo huku akifafanua kuwa kila mtu anayemiliki kipande cha ardhi nchini ni mapangaji wa ardhi hivyo anapaswa kulipa kodi.

Hata hivyo amesema Wizara ina mkakati wa kwenda nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinachodaiwa wanakipelekea hati ya madai ambapo amesema hatua hiyo inatarajiwa kuzaa matunda kama ambavyo imekuwa ikitumika.