December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasimamizi wa Uchaguzi Kata ya Kwashemshi, Korogwe wafundwa

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Korogwe

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani amewataka Wasimamizi Wasaidizi wa vituo vya kupiga kura kwenye Uchaguzi mdogo wa Kata ya Kwashemshi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Amesema moja ya kazi yao ni kuhahakisha hawaleti taharuki kwenye uchaguzi huo, na kusema mgombea atakaeshinda basi ashinde kwa halali.

Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Kwashemshi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakila kiapo mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe Vijijini na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani (hayupo pichani)katika mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi hao yanayofanyika Chuo cha Ualimu Korogwe.

Ameyasema hayo Julai 10, 2023 wakati anafungua mafunzo ya siku mbili kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na Makarani waongozaji wapiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Kwashemshi Wilaya ya Korogwe.

Magani amesema washiriki wa zoezi hilo wamekula kiapo ili kufanya kazi hiyo ya kusimamia zoezi la upigaji kura.

Ni matumaini yake wote watafanya kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu, na bahati nzuri karibu asilimia 99.9 wameshiriki shughuli kama hiyo siku za nyuma, hivyo yeyote atakaejaribu kuharibu, watamuweka pembeni.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe Vijijini na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani (kushoto), akiwaongoza kuapa, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kwashemshi kwenye halmashauri hiyo (hawapo pichani). Ni kwenye mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi hao yanayofanyika Chuo cha Ualimu Korogwe. Wengine ni Ofisa wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Samina Gullam (katikati), na Ofisa Ugavi Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Eva Swai (kulia).

“Zoezi hili ukiharibu kidogo madhara yake ni makubwa,kunahitajika umakini mkubwa Kwenye hili zoezi tukiona unataka kutuharibia tunakuweka pembeni,mmekula kiapo ili kutunza siri, na kama huna uwezo wa kutunza siri, tueleze tukuweke pembeni, usije ukasababisha uchaguzi kurudiwa”

“Tunataka mfanye kazi kwa ushirikiano ili kuona zoezi hili linakwenda vizuri. Usije ukaharibu, maana kosa moja ukilifanya, uchaguzi wote unaweza kurudiwa. Hivyo tunataka ufanye kazi hii bila kuleta taharuki kwenye jamii, na atakaeshinda ashinde kwa halali,”amesema Magani.

Magani amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwataka wajue wajibu wao kama Makarani waongozaji wapiga kura na taratibu za uchaguzi, hivyo ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo kila mmoja ataelewa majukumu yake, na kufanikisha uchaguzi huo.

Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Kwashemshi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakiwa kwenye mafunzo ya siku mbili yanayofanyika Chuo cha Ualimu Korogwe.

Akizungumza nje ya mafunzo hayo ya siku mbili, Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Samina Gullam amesema uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kwashemshi (CHADEMA) Twahiru Tindikai kujihudhuru na kutimkia CCM.

CCM imempa nafasi nyingine Tindikai, ambapo yeye ndiyo atapeperusha bendera ya chama hicho

Wagombea watano wameingia kwenye kinyang’anyiro hicho, ambapo uchaguzi huo utafanyika Julai 13, 2023 siku ya Alhamisi ambao ni Said Ngoma wa ADC, Majaliwa Kipepe wa ACT- Wazalendo, Hozza Hozza wa DP, na Juma Gao kwa tiketi ya ADA TADEA